Yanga ilivyofia tutani Singida


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wameondolewa katika mashindano ya Kombe la FA baada ya kukubali kutolewa kwa matuta 4-2 dhidi ya wenyeji Singida United katika mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Namfua mkoani hapa.
Kwa matokeo hayo, Singida United inayodhaminiwa na Kamapuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, na kunolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm, imetinga hatua ya nusu fainali na sasa itakutana na JKT Tanzania ya jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine ya hatua ya nusu fainali itawakutanisha Stand United ya Shinyanga dhidi ya Mtibwa Sugar kutoka Manungu, Morogoro ambayo ilisonga mbele baada ya kuifunga Azam FC kwa penalti 9-8 katika mchezo mwingine wa michuano hiyo uliopigwa juzi usiku.
Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Yusuph Mhilu ambaye alifunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na mshambuliaji mahiri wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu katika dakika ya 23.
Bao hilo lilidumu mpaka kipindi cha kwanza cha mchezo huo ulioanza kuchezwa huku mvua ikinyesha, na katika kipindi cha pili Kenny Ally aliisawazishia Singida United katika dakika ya 47 baada ya kufanikiwa kuwazidi mbinu mabeki wa Yanga.
Penalti za Singida United zilifungwa na Shafiq Batambuze, Tafanywa Kutinyu, Kenny Ally na Elinywesa Simbu ambaye aliingia uwanjani zikiwa zimebakia sekunde chache kabla ya dakika 90 kumalizika huku Antir Malik akikosa.
Wachezaji wa Yanga waliopata penalti ni Kelvin Yondani na Gadiel Michael huku Pappy Tshishimbi aliyekuwa wa kwanza kupiga penalti akipaisha na kipa wa Singida United, Ally Mustapha "Barthez" akipangua ya Emmanuel Martin.
Hata hivyo, Singida United ndiyo walifanya mashambulizi zaidi katika kipindi cha kwanza, lakini washambuliaji wake walishindwa kuwa makini kila walipofika kwenye eneo la 18 huku changamoto nyingine ikiwa ni maji ya mvua ambayo yalipoozesha mchezo huo.
Wenyeji hao walikaribia kupata bao katika dakika ya 28 kupitia kwa Tafandwa Kutinyu, lakini shuti lake alilopiga lilitoka pembeni na dakika mbili baadaye Kennedy Juma naye alipiga nje kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Kigi Makasi na kuinyima timu yao nafasi ya kufunga.
Bingwa wa michuano hiyo atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hapo mwakani.
Kwa matokeo hayo, Yanga ambayo nayo inadhaminiwa na SportPesa, sasa italazimika kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani.
Chanzo: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako