Winnie Mandela afariki dunia akiwa na miaka 81


Winnie Mandela, mke wa zamani wa Nelson Mandela, ambaye pia alipigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini amefariki dunia akiwa na miaka 81.
Habari za kifo chake zimethibitishwa na msaidizi wake.
Winnie alizaliwa mnamo 26 Oktoba mwaka 1936, na ingawa yeye na mumewe - Nelson Mandela - walitalikiana mapema miaka ya 1990, Winnie Madikizela Mandela kama alivyofahamika rasmi alisalia kutoa mchango katika maisha ya Bw Mandela.
Alikuwepo na walishikana mikono alipokuwa akiondoka gerezani baada ya kufungwa kwa miaka 27.
Msemaji wa familia Victor Dlamini amesema kupitia taarifa kuwa: "Amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, ambapo amekuwa akiingia na kutoka hospitalini mara kwa mara tangu mwnazo wa mwaka.
"Alifariki kwa amani mapema Jumatatu adhuhuri akiwa amezungukwa na familia na wapendwa wake."
Askofu mstaafu na mshindi wa tuzo ya Nobel Desmond Tutu amemsifu kama "ishara kuu ya vita dhidi ya ubaguzi wa rangi," kwa mujibu wa AFP.
Winnie alikuwa na miaka 20 hivi pale alipojiingiza katika siasa.
Alisomea kazi ya utoaji huduma za kijamii na haraka aliyazoea maisha ya kuwa mama na mwanasiasa.
Katika kipindi chote cha miaka 27 mumewe alipokuwa gerezani bila matumaini ya kuachiwa huru kutokana na hukumu ya kifungo cha maisha jela alichopewa mwaka 1964, Bi Winnie alilazimika kubeba jukumu la ulezi wa watoto na pia kuendeleza kampeni za kisiasa kutaka mashujaa wa kupigania nchi yao waachiwe huru hasa mumewe.
"Kamwe hatutapoteza matumaini na watu wangu hawatapoteza matumaini kamwe, bila shaka tunatarajia kwamba kazi itaendelea," alisema wakati huo.
Kutokana na hayo Bi Winnie Mandela alilazimishwa kusalia tu huko Brandford katika jimbo lao la Orange Free katika miaka ya 70 baada ya operesheni mojawapo za kupambana na ubaguzi wa rangi zilizokuja kujulikana zaidi kama the Soweto Uprising.
source:bbc
Na: sabby@spoti.co.tz
MaoniMaoni Yako