Tuesday, April 3, 2018

VIDEO: Simba ya Al Masry yaishukia Njombe Mji

Tags

Dar es Salaam. Mbio za ubingwa zimeshika kasi baada ya kocha wa Simba, Pierre Lechantre kuanza na mfumo na wachezaji wale waliocheza na Al Masry dhidi ya timu Njombe Mji leo saa 10:00 jioni, kwenye Uwanja wa Sabasaba.
Mfaransa Lechantre alitumia mfumo wa 3-5-2 katika mchezo dhidi ya Al Masry na vinara hao kuonyesha soka la kiwango cha juu pamoja na kutolewa na Wamisri kwa sheria ya bao la ugenini katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kocha wa Simba, Lechantre anajua sasa upinzani wa kuwania ubingwa umeongezeka baada ya Yanga kutolewa katika Kombe la FA, ili kujiweka salama ni lazima kuhakikisha anashinda kila mchezo wa mbele yake kwa kuanzia na Njombe Mji.
Simba wanahitaji matokeo mazuri ili kujihakikishia wanawaacha wapinzani wao Yanga, kwa tofauti kubwa ya pointi, huku Njombe wakihitaji ushindi ili kutoka katika hatua ya kushuka daraja msimu huu.
Katika kikosi cha Simba kinachocheza leo dhidi ya Njombe, ndio kikosi ambacho kilicheza katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.
Katika mchezo wa hapa nyumbani walitumia mfumo huu huu wa 3-5-2, kipa akianza Aish Manula, mabeki wakiwa Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili na Juuko Murshid, huku akiwatumia Nicholas Gyan na Asante Kwasi kama Mawinga wanaopita kupeleka mashambulizi kwa kutumia kasi yao.
Viungo walicheza James Kotei, Shomari Kapombe na Shiza Kichuya, ambapo walionekana kuelewana vilivyo na Kapombe kuimudu nafasi ya kiungo mkabaji akisaidiana na Mghana  Kotei, huku washambuliaji wakisimama kama kawaida Emmanuel Okwi na John Bocco.
Kikosi hicho ndicho ambacho kinaenda kuanza dhidi ya Njombe, hivyo kwa jinsi ambavyo Simba walicheza dhidi ya Al Masry na kutoka sare ya 2-2 kwa timu kama ile, leo tutarajie mchezo mzuri katika timu hizi ambazo zote zinatafuta nafasi ya kukaa sehemu nzuri kabla ya ligi kumalizika msimu huu.
Kikosi cha Simba kinachoanza: Aish Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Juuko Murshid, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya.
Kikosi cha Njombe: David Kisu, Christopher Kasewa, Stevin Mwaijala, Hussen Akilimali, Peter Mwangosi, Jimmy Mwasondola, Awadh Salum, Mustapha Bakari, Ethiene Ngladjoe, David Obash na Ditram Nchimbi.


Chanzo: Mwananchi
==>>Unaweza Kudownload  APP yetu ya SPOTI << kwa Kubofya Hapa>>