VIDEO: Simba waifanyia Yanga kitu mbaya kilio kila kona


Dar es Salaam. Beki Erasto Nyoni amepeleka kilio Jangwani baada ya kuifungia Simba bao pekee ikichapa Yanga 1-0 leo, Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba kuongoza ligi kwa kufikisha pointi 62, hivyo wanahitaji pointi tano tu katika mechi zake nne zijazo ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano ya kusubili.
Nyoni alifunga bao hilo dakika 35, akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Shizza Kichuya uliomgonga kiungo wa Yanga, Raphael Daud na kumkuta beki huyo wa Simba akiwa peke yake na kutumbukiza wavuni.

 Kabla ya bao hilo nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani alimchezea vibaya beki wa Simba, Shomari Kapombe na kusababisha adhabu hiyo iliyozaa goli.

Yanga ilipata pigo mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya beki wake Hassan Kessy kupewa kadi nyekundu ikiwa ni kadi ya pili ya njano kwa kumchezea vibaya beki wa Simba, Asante Kwasi.
Awali nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani alinusurika kupata kadi nyekundu kutokana na kitendo chake cha kumtemea mate beki wa Simba, Kwasi, lakini mwamuzi hakuona tukio hilo pamoja na Mghana huyo kumlalamikia.
 Simba ilitawala mchezo huo na kufanikiwa kupata kona nane, wakati Yanga imeweka rekodi ya kucheza dakika 90, bila ya kupiga kona yoyote katika mchezo wa watani wa jadi.
Yanga imefanywa mabadiliko dakika ya 46 kwa kumtoa Rafael Daud na kumwingiza Juma Mahadhi, pia dakika 62 kwa kumtoa Ibrahim Ajib na nafasi yake ikachukuliwa na Pius Buswita.
Mabadiliko ya kutoka kwa Ajib ni kama mashabiki wa  Simba waliyafurahia kwani walikuwa wakishangilia na kupiga makofi.
Pia,  dakika ya 80 alimtoa Tshishimbi na kumwingiza Emmanuel Martin, mabadiliko ambayo yaliwashangaza mashabiki wengi kutokana na namna wanavyomwamini mchezaji huyo.
Simba wao wamefanya mabadiliko mara moja kwa kumtoa Nicholas Gyan ambaye alikuwa anacheza beki ya kulia akaingia Paul Bukaba.

Hata hivyo Yanga iliwabidi wacheze pungufu kwa dakika 42 baada ya beki wao Hassan Ramadhan Kessy kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kutoka Mwanza katika dakika ya 48.
Kadi hiyo ni jumla ya kadi za njano mbili. Hiyo ya pili ni baada ya kumchezea vibaya Kwasi kwa kumkata ngwala.
Yanga walipambana na kutengeneza nafasi nzuri dakika ya 52 kama shuti lililopigwa na Tshishimbi katikati ya uwanja nje kidogo ya D ya golini angelipiga kwa nguvu ingekuwa bao lakini kwa sababu halikuwa la nguvu Aishi alilidaka kwa urahisi kabisa.
Mashabiki Simba wauteka uwanja
Mpaka saa tisa jioni, mashabiki wa Simba walikuwa wengi zaidi ya Yanga na ndiyo wanaonekana kushangilia kwa shangwe kuliko watani wao.
Mashabiki hao wamejitokeza kwa wingi na kujaza viti vya upande wao huku upande wa Yanga ukionekana kuwa na idadi ndogo ya watazamaji.
Wakiwa katika mavazi yao ya rangi nyekundu na nyeupe wanaonekana kushangilia kwa shangwe.
VIKOSI
Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, James Kotei, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, 1John Bocco,  Shiza Kichuya

Yanga: Youth Rostand, Hassan Ramadhan, Gadiel Michael,  Andrew Vincent,  Kelvin Yondani, Juma Makapu,  Yusuph Muhilu, Papy Tshishimbi,  Obrey Chirwa, Raphael Daud,  Ibrahim Ajib.
Credit to Azam TV and Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako