UKUTA YANGA PASUA KICHWA


ZIKIWA zimebakia saa chache kabla ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara hawajakutana na Welayta Dicha FC kutoka Ethiopia, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, amesema kuwa kutowaruhusu wapinzani wao kupata bao lolote hapa nyumbani ni moja ya mipango waliyoiandaa.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa itawakaribisha Welayta Dicha FC katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Africa utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Nsajigwa aliliambia gazeti hili jana kuwa mbali na kusaka mabao ya mapema, kuruhusu mpinzani kukufunga nyumbani kwenye mashindano hayo ya kimataifa ni sawa na kujiweka "njia panda".
Alisema kuwa nguvu ya kusaka mabao inatakiwa ilingane na ile ya kuzuia mpinzani asipate bao na endapo wakifanikiwa kutimiza malengo hayo, anaamini kikosi chake kitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya Welayta Dicha FC ya Ethiopia.
"Moja ya mambo ambayo tunatakiwa kuhakikisha tunafanya hapa nyumbani ni kutokubali kufungwa, hata kama ni bao moja, haitakiwi, tunahitaji kuwa na nguvu sawa kwenye safu ya ushambuliaji na safu ya ulinzi, tunawakumbusha kuwa makosa ya kwenye ligi tusiyarudie," alisema beki huyo wa zamani wa Yanga.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa, amesema kuwa klabu hiyo inashindwa kutuma barua CAF ili kupata ufafanuzi juu ya adhabu ya kumkosa Yondani na kueleza kuwa kocha wao, George Lwandamina, amesema nyota huyo hana kadi mbili za njano kama ilivyoripotiwa.
"Ni kweli kocha ametueleza, lakini sisi kama Yanga hatuna video yoyote ambayo itatuthibitishia kama alipata au hakupata, na taarifa rasmi inayowataja wachezaji hao wanne hatujaipata, na ukiangalia muda uliobakia ni mdogo," alisema Mkwasa.
Mkwasa alikiri kuwa kukosekana kwa wachezaji hao wa kikosi cha kwanza katika mechi ya kesho ni "pigo" katika timu yao kwa sababu nyota hao wanauzoefu wa kupambana na wapinzani.
Wachezaji ambao watakosekana katika mchezo huo kuwa ni pamoja na Kelvin Yondani, Obrey Chirwa, Pappy Tshishimbi na Said Makapu.
Katika kujiandaa na mchezo huo, Yanga ambayo Jumapili iliyopita ilitolewa katika mashindano ya Kombe la FA na timu ya Singida United, imeweka kambi mkoani Morogoro  na inatarajia kurejea jijini leo mchana kuwavaa Wahabeshi hao ambao waliwasili nchini jana mchana.
Chanzo: IPP Media
MaoniMaoni Yako