Twiga Stars yalazimishwa sare na Zambia ‘Shepolopolo’ Taifa

TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imejiweka vibaya katika kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AWC) Ghana Novemba mwaka huu kwa kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya wenzao wa Zambia (Shepolopolo) katika mechi iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Twiga Stars inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 4-4 katika mechi ya marudiano itakayofanyika mjini Lusaka, Zambia Aprili 8 mwaka huu ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo
Mabao ya Twiga Stars katika mchezo huo yalifungwa na Stumai Abdallah na Asha Rashid 'Mwalala' ambaye alipachika mawili.
Kwa upande wa Shepolopolo waliofunga ni Barbra Banda aliyefunga mawili na lingine likipachikwa na Misozu Zulu.
Hadi wanakwenda mapumziko, Twiga Stars inayofundishwa na Kocha Sebastian Mkoma na Edna Lema 'Mourinho' ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Shepolopolo ilifanya mashambulizi zaidi ukilinganisha na wenyeji lakini kipa wa Twiga Stars, Fatuma Omary, alijitahidi kudaka mashambulizi na kuisaidia timu yake katika mechi hiyo iliyochezeshwa na waamuzi kutoka Chad.
Baada ya mechi kumalizika, wachezaji wa Shepolopolo ambao walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kenya na kufungwa 3-0, walianza kucheza "ndombolo" ishara ambao wamefurahia matokeo hayo ya ugenini ambayo kwao ni mazuri.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zinatarajiwa kufanyika Novemba na Desemba mwaka huu jijini Accra, Ghana wakati zile za dunia zitafanyika mwakani Paris, Ufaransa.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Fatuma Omary, Wema Richard, Happy Hezron, Fatuma Issa, Sophia Mwasikili/Esther Mayala dk52, Evellyne Sekikubo, Stumai Abdallah, Deonisia Daniel, Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’ na Amina Ally/Christina Daudi dk75.  
Zambia; Catherine Nusinda, Margareth Belemu, Jane Chalwa/Jackline Nkole dk51, Chisamu Lwendo, Anitha Mulenga, Rhoda Chileshe, Misozi Zulu, Barbra Banda, Rachael Kundananji, Hellen Chanda na Theresia Chewa/Marry Mambwe dk46.
 
by richard@spoti.co.tz 
MaoniMaoni Yako