Simon Msuva Akabidhiwa Mikoba na klabu yake ya Difa El Jadida ya Morocco.

HATIMAYE mshambuliaji wa Taifa Stars, Saimon Msuva amepewa rasmi majukumu ya kupiga mikwaju ya penalti kwenye klabu yake ya Difa El Jadida ya Morocco.

Msuva amepewa majukumu hayo na mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Morocco, Abderrahim Taleb ambaye kwa sasa ndiye kocha wa kikosi hicho chenye maskani yake, mjini Jadida.
Akizungumzia majukumu hayo mapya ambayo pia alikuwa nayo alipokuwa akiichezea Yanga, Msuva alisema anataka kuitumia nafasi hiyo kuendelea kuisaidia Difaa kufunga mabao zaidi kila watakapokuwa wanapata penalti.
“Ilichukua muda mpaka nimepewa majukumu hayo, lakini kinachonifurahisha ni kwamba ndani ya msimu wangu wa kwanza wameniamini na kunipa hilo jukumu hilo zito.
“Nimekuwa nikifanya vizuri kwenye upigaji wa matuta kwenye mazoezi pengine hilo limechangia kocha kuniteua kuwa mpiga wa penalti za ndani ya mchezo, nilipiga kwenye mchezo uliopita na nilifunga lakini kwa sasa imekuwa rasmi,” alisema mshambuliaji huyo.
Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Raja Casablanca, Msuva amefunga mabao manane, Ligi Kuu Morocco ambayo pia inafahamika kama Batola Pro.
Mabao hayo manane yamemfanya Msuva kuachwa nyuma kwa mabao sita na kinara wa ufungaji wa Batola Pro, Mouhcine Lajour anayeichezea Raja Casablanca akiwa na mabao 14.
Kwa uteuzi huo, Msuva anaamini anaweza kufanya vizuri zaidi akiahidi kujituma na kuongeza juhudi mazoezini na kwenye mechi ili kusaidia timu yake.
Source: Mwanaspoti