Thursday, April 5, 2018

SIMBA: Yanga wanatishia ubingwa wetu

Tags

Uongozi wa Simba umeingiwa na hofu na Yanga na kudai sasa vita ya ubingwa wa ligi kuu imekolea, baada ya wapinzani wao hao kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la FA.
Yanga imetolewa kwenye michuano ya FA juzi na Singida United na sasa imesalia kwenye ligi kuu pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika huku Simba ikiwa inashiriki ligi kuu pekee.
Simba na Yanga katika ligi kwa sasa zote zina pointi 46, zikitofautiana kwenye mabao ya kufungwa na kufunga na Simba akiwa
na mechi kumi, Yanga amesalia na michezo tisa kuweza kumaliza ligi.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema kuwa kwa sasa vita imekuwa ngumu na kila timu inasaka tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Kwa sasa vita ya ubingwa wa ligi kuu imekuwa ngumu, inabidi kupambana kweli kuweza kupata matokeo sababu kama mlivyoona wapinzani wetu wametolewa kwenye FA ambapo nadhani walitegemea ubingwa lakini ndiyo hivyo kutolewa kwao kule ni wazi imekuwa vita kati yetu.
“Na sisi wote tunapambana kuhakikisha moja wetu aweze kupata tiketi ya kuweza kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, sasa wanatutisha na tunatakiwa kuongeza kasi sana.
“Lakini wapinzani wetu licha ya kuwepo kwenye ligi pia wanaweza kupambana labda hata wakaweza kuchukua ubingwa kwenye michuano ya CAF ambayo sisi tuliweza kutolewa mapema,” alisema Manara.
Baada ya kupita miaka mingi msimu huu ulikuwa wa kwanza kwa timu za Simba na Yanga kushiriki michuano ya kimataifa pamoja ambapo Yanga walishiriki Klabu Bingwa Afrika na Simba Kombe la Shirikisho.
CHANZO: CHAMPIONI
Na: Agape Patrick
Email: agape@spoti.co.tz