Simba: Vitendo vitaongea Bara


KIKOSI cha Simba ya jijini Dar es Salaam kinatarajia kuwasili Morogoro leo tayari kuwavaa wenyeji Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kufanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo, imeelezwa jana.
Simba itawasili Morogoro ikitokea Iringa ambapo iliweka kambi ya muda baada ya kumaliza mechi yake dhidi ya Njombe Mji iliyofanyika mapema wiki hii kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema kuwa waliamua kubaki Iringa ili kutoa nafasi kwa wachezaji kujifua katika mazingira ya baridi ambayo ni bora zaidi ukilinganisha na hali ya hewa ya Dar es Salaam.
Djuma alisema kuwa ligi imeingia katika hatua ya lala salama na wanahitaji kuona wachezaji wote wanakuwa tayari kwa mapambano kwa ajili ya kuchukua pointi tatu kila wanaposhuka uwanjani.
"Umefika muda wa hatari, tunahitaji kuonyesha vitendo uwanjani, kule ndio kunaongea zaidi," alisema kwa kifupi kocha huyo.
Aliitaja Mtibwa Sugar kuwa ni moja ya timu ngumu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara na kwa sababu hiyo wataingia uwanjani kwa tahadhari huku wakiwaheshimu wapinzani wao muda wote wa mchezo.
"Kama tulivyocheza kwa heshima dhidi ya Njombe Mji, tutaendelea kufanya hivyo tutakapocheza na Mtibwa Sugar, tofauti ni majina, lakini wote tunacheza ligi moja na unaposhinda unapata pointi tatu," Djuma aliongeza.
Baada ya mechi hiyo, Simba itarejea jijini kuwasubiri Mbeya City na Tanzania Prisons, mechi zote zikipangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Simba ndio vinara wa ligi hiyo yenye timu 16 ikiwa na pointi 49 ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 46 wakati mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC ambao keshokutwa wataikabili Mbeya City jijini Mbeya wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 40.
Chanzo: IPP Media

MaoniMaoni Yako