Monday, April 2, 2018

She-polopolo waifuata Twiga Stars

Tags


KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Zambia maarufu She-polopolo, kinatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya kuwavaa wenyeji wao, Twiga Stars, imeelezwa jijini Dar es Salaam jana.
Twiga Stars inatarajia kuwakaribisha She-polopolo katika mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWC) utakaopigwa keshokutwa, Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.
Amina Karuma, Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA), aliliambia gazeti hili jana kuwa wapinzani wao wanawasili nchini leo mchana na maandalizi ya mechi hiyo yako katika hatua za mwisho.
Karuma alisema pia waamuzi watakaochezesha mechi hiyo waliwasili jana huku kamisaa akitarajiwa kutua nchini leo mchana.
"Kwa upande wa utawala kila kitu kinakwenda vizuri, tumejipanga kuwapokea wageni wetu kama taratibu za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) zinavyoeleza, timu yetu pia inaendelea vyema na mazoezi yake kwa ajili ya kuhakikisha tunaanza vyema kampeni hii," alisema Karuma.
Kiongozi huyo amewaomba mashabiki wa soka kujitokeza kuishangilia timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Taifa Stars ilipowakaribisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mechi ya kirafiki iliyomalizika kwa kupata ushindi wa mabao 2-0.
Mwaka 2010, ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Boniface Mkwasa, Twiga Stars ilifanikiwa kushiriki fainali za Afrika katika michuano iliyofanyika Afrika Kusini.
Chanzo: IPP Media