Pilau la Pasaka ‘ladoda’ Yanga


Sikukuu ya Pasaka imekuwa mbaya kwa upande wa Yanga baada ya kuondoshwa kwenye kombe la Azam Sports Federation Cup na Singida United kwa mikwaju ya penati 4-2 kufuatia timu hizo kutoka sare ya kufungana 1-1 ndani ya dakika 90.
Mwaka wa tabu majanga huwa hayaishi, vigogo wa soka la Tanzania bara wote wameshaaga mashindano hayo walianza Simba, wakafuata Azam na Yanga wanakamilisha.
Singida wanafuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza kwa kutupa nje Yanga ambayo ilishinda taji hilo mwaka 2016 kwa kuifunga Azam kwenye mchezo wa fainali.
Timu zilizofuzu hatua ya nusu fainali ya ASFC ni Stand United, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar na Singida United. Katika hatua hiyo, Stand United itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar huku JKT Tanzania ikicheza dhidi ya Singida United.
Penati za Singida United zimefungwa na Batambuze, Kutinyu, Kenny na Sumbi lakini Antiri mkwaju wake uliokolewa na golikipa wa Yanga Youthe Rostand.
Wachezaji wa Yanga waliofanikiwa kufunga penati ni Yondani na Gadiel wakati Tshishimbi na Martin wakikosa.

MaoniMaoni Yako