Okwi, Bocco mtegoni Jangwani


Dar es Salaam. Simba imetua jijini Dar es salaam na leo itaendelea na mazoezi yao kwenye Uwanja wa Boko Veterani, ikitokea mjini Morogoro ili kuiwinda Yanga watakaovaana Jumapili hii, lakini nyota wake wakiwamo vinara wa mabao Emmanuel Okwi na John Bocco wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa katika mechi hiyo ya watani.
Okwi na Bocco wana kibarua cha kupunguza idadi ya mabao ambayo timu yao ya Simba inadaiwa na watani zao Yanga tangu walipoanza kuvaana katika mechi za Ligi Kuu kuanza mwaka 1965.
Rekodi zinaonyesha kuwa, katika mechi zao 99 zilizopita za watani Yanga imefunga mabao 107, huku yenyewe ikiruhusu mabao 95 ikiwa na maana Simba ina deni la jumla ya mabao 12 ambalo Okwi na Bocco na ikiwezekana Shiza Kichuya wanapaswa kulipa.
Mbali na kazi kubwa ya kusaka mabao ya kupunguza pengo lao na watani zao, pia nyota wa Simba na kibarua kingine cha kuhakikisha wanapunguza pengo la ushindi baina yao na Yanga.
Simba katika mechi hizo 99 baina yao na Yanga wameshinda 29, huku wakikubali kipigo katika mechi 36, saba zaidi ya Vijana wa Jangwani, huku mechi zao 34 zikiisha kwa sare.
Katika mechi ya mkondo wa kwanza ambao Simba ililazimisha sare ya Yanga waliokuwa wenyeji, bao lao lilifungwa na Kichuya, huku Yanga ikisawazisha kupitia kwa Obrey Chirwa mwenye mabao 12 mpaka sasa katika ligi ya msimu huu.
Bocco na Okwi wamezalisha jumla ya mabao 33, Okwi akifunga 19 akiwa kinara na nyota mwenzake akifuatia nyuma yake akitupia kambani mabao 14.
Nyota hao wa Simba na hata wale wa wapinzani wao akiwamo Chirwa, Ibrahim Ajibu na wengine wa Jangwani wana kazi kubwa ya kuwa wachezaji wa kwanza baada ya miaka 40 kufunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo mmoja.
Rekodi ya hat trick katika mechi ya watani iliwekwa mnamo Julai 19, 1977 Abdallah 'King' Kibadeni alipoyafunga wakati Simba wakiandikisha historia walipoifunga Yanga mabao 6-0, kipigo ambacho mpaka leo Jangwani wanahaha kukirudisha bila mafanikio.
Msimamo mechi za watani tangu 1965
                 P     W    D     L      F      A     PTS
YANGA   99   36   34   29   107 95   142
SIMBA    99   29   34   36   95   107 121
Chanzo: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako