Mfaransa hataki mchezo Simba


MFARANSA wa Simba, Pierre Lechantre buana, kumbe hataki utani kabisa, kwani jana asubuhi wakati kikosi chake kikianza safari kuelekea Njombe kuwafuata Njombe Mji aliamua kufanya jambo moja ambalo mashabiki wa Simba huenda wasiamini.
Kocha huyo mapema asubuhi kabla ya safari hiyo watakayofikia kwanza Iringa kabla ya kuutafuta mji wa Njombe, alitangaza majina ya wachezaji 22 na kuwapiga chini wengine wanne waliokuwa na matumaini ya kuwepo kwenye msafara huo.
Mastaa hao wanne ambao Lechantre hakuwajumuisha ni pamoja na kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto, mabeki wa pembeni, Jamali Mwambeleko na Ally Shomary, Kipa Emmanuel Mseja na kiungo mshambuliaji Mohammed Ibrahim ‘MO’ waliobaki jijini Dar.
Wachezaji hao ambao walitemwa wanaungana na waliotoka majeruhi akiwamo Haruna Niyonzima na Salum Mbonde ambao wanaendelea kukusanya nguvu kabla ya kuanza kupewa majukumu katika mechi zilizosalia za VPL.
Wachezaji wao walikuwa na matumaini ya kuambatana na timu kutokana na mazoezi makali waliyopiga mara ya mwisho juzi jioni kabla ya timu kujichimbia kambi ya muda mfupi ya Sea Scape na baadhi yao akiwamo Mwambeleko amekubali yaishe.
Mwambeleko aliyetua Msimbazi msimu huu akitokea Mbao FC, alisema hana kauli kwa kuwa maamuzi ya kocha juu ya nan i awepo kikosini ni kocha, japo alikuwa na hamu ya kuitumikia timu yake katika mechi hiyo ya ugenini itakayopigwa Jumanne.
“Kwa upande wangu nilikuwa nafanya mazoezi kwa nguvu zote ili Lechantre aweze kunifikiria, huenda hajaridhishwa na kiwango na sasa naendelea kujifua mazoezi binafsi ili wakirudi safari niweze kumridhisha mwalimu, nina hamu ya kuingia kikosini,” alisema.
“Kiukweli nimeumia, ila sina jinsi zaidi ya kupambana zaidi na kuhakikisha napata nafasi ya kucheza ingawa nafasi ambayo nacheza tupo wachezaji watatu,” alisema.
OKWI KATISHA
Katika mazoezi ya Simba ambayo walifanya kwa mara ya mwisho juzi Ijumaa jioni katika uwanja wa Boko Veterans kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara, Emmanuel Okwi hakuwepo kwa maelezo alikuwa kwao Uganda lakini alitua na kuwepo katika msafara.
Okwi aliwasili kambini katika Hotel ya Sea Scape usiku wa juzi na jana aliungana katika msafara na wenzake na kuondoka wote Njombe.
“Kweli hakuwepo mazoezi ya mwisho tuliofanya Dar es Salaam lakini tulishawasilina nae na aliingia kambini na tupo naye kwenye msafara, ila sijui kwanini Juuko Murshid alichelewa japo waliondoka wote kwenda kulitumikia taifa lao,” alisema mmoja wa vigogo wa Simba.
MSIKIE MRUNDI
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma alisema walikaa na Lechantre waliona ni vyema kufikia Iringa kwa siku moja ili wachezaji wazoee mazingira ya baridi na siku inayofuata yaani kesho waingie Njombe kwani si mbali na hapo. Lengo ni kuhakikisha tunashinda mchezo wetu muhimu.”
Chanzo: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako