Kwa rekodi hizi, Yanga hawana Cha Kuwafanya Simba msimu huu!!

INAWEZEKANA Yanga bado inawachukulia Simba poa, lakini ukweli watani zao hao kwa msimu huu wapo vizuri kinoma na kama Jangwani wakizubaa tu, taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu Bara wanaolishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo litayeyuka na kutua Msimbazi.
Ipo hivi. Mastaa watatu tu wa Wekundu hao wa Msimbazi; Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya kazi yao msimu huu ni sawa na iliyofanywa na wachezaji wote wa Yanga.
Watatu hao wamefunga mabao 40, idadi ambayo ni zaidi ya yale yanayomilikiwa na kikosi kizima cha Yanga mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara.
Chukua mabao 12 ya Obrey Chirwa na mengine 26 yaliyofungwa na nyota wengine 10 yakiwamo saba ya Ibrahim Ajibu yanaifanya Yanga kuwa na mabao 38.
Kuna mengine mawili wamesaidiwa na wachezaji wa timu pinzani ndio wanayafikia mabao ya nyota hao watatu wa Simba ambao keshokutwa Jumapili wataanza kwenye kikosi cha kwanza.
Yaani idadi ya mabao ya Okwi, Bocco na Kichuya pale Yanga imefikiwa kwa kufungwa na nyota 11 ambao ni sawa na kikosi kizima.
Ukiachana na Chirwa aliyefunga 12, mabao mengine ya Yanga yaliyopatikana katika mechi 23 za msimu huu, yaliwekwa kimiani na Ajibu mwenye saba, Emmanuel Martin na Pius Busitwa ambao kila mmoja amefunga manne na matatu ya Papy Kabamba Tshishimbi.
Donald Ngoma na Yusuf Mhilu kila mmoja amefunga mabao mawili, huku mabeki Hassan Kessy, Gadiel Michael na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na kiungo Rafael Daud kila mmoja akifunga moja na mabao mengine ya Yanga yalifungwa na mabeki wa timu pinzani.
Nahodha wa Prisons Laurent Mpalile aliifungia Yanga bao katika sare ya 1-1 katika mechi yao iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex, huku Juma Shemvuni wa Kagera Sugar naye akijifunga kwenye ushindi wa Yanga wa mabao 3-0 na kukamilisha idadi ya mabao 40 yote ya Yanga ya msimu huu.
Kwa nyota hao wa Simba, Okwi ndiye anayewakimbiza akiwa na mabao 19, huku Bocco akimfuata na mabao yake 14 na Kichuya akikwamisha mengine saba.
Safu hiyo ya ushambuliaji ya Simba pia imeiacha mbali Azam FC yenye mabao 24 kwa timu nzima msimu huu ikiwa imeshuka uwanjani mara 25.
Kwa upande wa timu zote za Ligi Kuu mpaka sasa zimefunga mabao 393, huku Simba peke yake ikiwa imefunga asilimia 15 ya mabao hayo.
CHAMBUA ANENA
Kasi hiyo ya Simba hasa kwa nyota hao watatu imemfanya nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua kukiri Yanga lazima ijipange kweli kweli kwenye mchezo wa Jumapili.
Chambua alisema Simba inaonekana kuwa kwenye ari nzuri ya kufunga kutokana na idadi ya mabao ambayo nyota wake wameyafunga hadi sasa msimu huu, huku wakitaka kubeba taji wanalolisaka kwa msimu wa sita sasa bila kulitia mkononi, mara ya mwisho kulibeba ilikuwa mwaka 2012.
“Safu ya Simba kwa sasa ipo vizuri kama ilivyo kuwa Yanga ambapo ilikuwa na Amissi Tambwe na Donald Ngoma, kila walipokuwa wakicheza mechi mtu uliamini timu itashinda zaidi ya mabao matatu,” alisema.
KAPOMBE APIGA DONGO
Beki wa Simba Shomary Kapombe amefichua kuwa mechi yao dhidi ya Yanga ndio inaweza kutoa taswira ya ubingwa msimu huu na wamejipanga kuhakikisha kuwatoa nishai wapinzani wao.
Kapombe alisema mazoezi waliyopata mjini Morogoro chini ya kocha Pierre Lechantre yanawapa jeuri ya kuamini kuwa, Yanga hawana chao katika mechi yao ya Jumapili.
“Kambi ilikuwa nzuri na tumefanya mazoezi ya kutosha yalifanya kila mchezaji kuwa na morali ya kutosha ili kuhakikisha tunaondoka na ushindi katika mechi hiyo,” alisema.
“Sikuwepo katika mechi ya kwanza nilikuwa majeruhi, lakini ni tumaini langu nitapata nafasi ya kucheza Jumapili na nitahakikisha napambana ili kuhakikisha tunashinda.”
MRUNDI AMALIZA KAZI
Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma, alisema kambi ilikuwa nzuri na wanatambua kuwa wana mechi kubwa mbele yao zitakazotoa mwanga wa ubingwa kwao msimu huu.
“Nafasi pekee iliyobaki kwetu ni kufanya vizuri ni ligi tu hatuna budi kujituma, kujitolea na kupambana mpaka dakika ya mwisho ili kupata matokeo ya ushindi,” alisema.
“Benchi la Ufundi tutamitiza majukumu yetu na umekuwa utamaduni wetu wa kuwaangalia wapinzani wanavyocheza katika kukaba na kushambulia, ndio maana tunabadilisha mbinu katika kila mechi na tutafanya hivyo katika mechi hiyo,” alisema.
Simba imerejesha kambi jijini Dar kutoka Morogoro.
Source: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako