Juventus 0-3 Real Madrid: Bao la Cristiano Ronaldo lililowafurahisha hata mashabiki wa Juventus

Cristiano Ronaldo alifunga mojawapo ya mabao bora zaidi katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa bao la kushangaza la 'bicycle-kick' na kuwasaidia Real Madrid kuwalawa Juventus katika mechi ya mkondo wa kwanza ya robofainali.
Ronaldo aliandika historia kwa mabao yote mawili.
Kwanza, alifikia krosi ya Isco na kufunga bao la Real la kwanza dakika ya 3 ambapo aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika mechi 10 mtawalia Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Juve walikuwa na nafasi ya kusawazisha kipindi cha kwanza ingawa Toni Kroos alikaribia pia kufunga kwa kombora kali lililogonga mwamba wa goli. Alipiga kiki hiyo akiwa hatua 25 kutoka kwenye goli.
Kisha, wakati wa 'mfalme' wa soka kutoka Ureno ukawadia.
Dani Carvajal alituma krosi eneo la hatari na Ronaldo akapaa juu angani na kutoa kiki kali ambayo ilimwacha kipa stadi wa Juve Gianluigi Buffon akiwa ameduwaa dakika ya 64.

Bao hilo lilikuwa la ustadi mkubwa kiasi kwamba mashabiki wa Juventus ya Italia, ambao bila shaka walivunjiwa matumaini ya kufika nusufainali na bao hilo, walisimama na kumshangilia Ronaldo.
Waitaliano hao walijipata wakitumbukia kwenye taabu zaidi baada ya Paulo Dybala kuoneshwa kadi ya pili ya manjano na kufukuzwa uwanjani dakika ya 66 kwa kumchezea visivyo Carvajal.
Marcelo alikamilisha ushindi dakika ya 72 kwa kucheza moja mbili na Ronaldo kabla ya kufunga.

Meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane alivyolipokea bao hilo la pili la Ronaldo ilitosha kufahamu ustadi uliotumiwa.
Alitingisha kichwa chake na kuonekana kupigwa na butwaa usoni, alipindua kichwa upande na kisha kuonekana kulikubali.
Katika maisha yake ya uchezaji alifunga mabao mengi ya kushangaza akiwa Turin mwenyewe, lakini alichokiona kutoka kwa Cristiano Ronaldo kilikuwa cha kipekee.
Ronaldo, 33, alikuwa ameruka juu kana kwamba ni kawaida yake tu na kuutuma mpira kimiani.
Baada ya mpira kutulia kwenye wavu, mashabiki wa Juve walimfuata Zidane na kusimama kumshangilia Ronaldo.
Winga wa zamani wa Scotland ambaye alikuwa akitangazia BBC Radio 5 live alishangazwa pia na Ronaldo.
"Unapoona mpira unaelekea kwake, unafikiria 'Oh, hautajaribu kuupiga mpira huyo kwa kuupitisha juu cha kichwa chako.' Kisha, pa! Unajionea mwenyewe, unatazama."
"Si jambo la kawaida. Watu wanazungumzia jinsi Ronaldo anazeeka sasa - lakini hakuna kasoro yoyote kwenye mwili wake iwapo anaweza kufanya jambo kama hilo. Alipima vyema kabisa, na ubunifu wa kufanya hivyo ni wa kushangaza."

posted by Lebabtv
Source: Bbc Swahili

MaoniMaoni Yako