Julio: Kutolewa Yanga, Simba, Azam ni ishara njema kwa soka Tanzania


Dar es Salaam. Nyota wa zamani Yanga na Simba wamesema kuingia kwa nusu fainali ya Kombe la FA timu za Mtibwa Sugar, JKT Tanzania, Singida United na Stand United ni ishara ya mwanzo wa zama mpya za soka la Tanzania.
Wachezaji hao wametoa kauli hiyo ikiwa ni mara tangu kurudishwa kwa mashindano hayo Yanga, Simba na Azam zimeshindwa kufuzu kucheza nusu fainali ya mashindano hivyo kupoteza nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' alisema ili soka la Tanzania lipige hatua ni lazima Yanga, Simba na Azam zipate ushindani halisi kama ilivyotokea kwenye Kombe la FA.
"Kwanza hizo timu kubwa zimekuwa zikishiriki mara kwa mara kwenye mashindano ya kimataifa, lakini zimekuwa hazifiki kokote.  Kuna wakati zimekuwa zikipata fursa hiyo huku zikiwa hazina ubora, lakini kwa hili la kutolewa katika Kombe la FA nadhani lina faida kubwa kwa soka letu.
“Naamini tutapata wawakilishi wapya ambao watakuwa na kiu ya kufika mbali zaidi tofauti na hizo timu tulizozioea ambazo kila wakati zimekuwa zikisindikiza wengine kwenye mashindano ya kimataifa. Angalau sasa tuone timu nyingine zitafanya nini huko," alisema Malima.
Kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema timu hizo kubwa kukosa nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho ni darasa kwa soka la Tanzania.
"Binafsi hii ni ndoto ambayo nilikuwa naiota kwa muda mrefu na leo hii hatimaye imetimia. Kwa muda mrefu Tanzania tumekuwa hatufanyi vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu kwa sababu timu ambazo zimekuwa zikishiriki ni zilezile na mbaya zaidi huwa zinafanya vibaya.
“Zimekuwa zikiridhika na kubweteka, lakini naamini kwa timu nyingine kupata nafasi awamu hii, itasaidia kuwajenga kisaikolojia wachezaji wa hizo timu, kupata uzoefu wa mechi za kimataifa sambamba na kujifunza masuala mbalimbali katika nchi za wenzetu jambo ambalo ni faida kwetu," alisema Julio.
Beki za zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa alisema," Kwangu kutolewa kwa hizo timu kubwa kama chachu ya kuleta mwamko kwa wachezaji wa timu nyingine ambao awali walikuwa wanaamini kwamba mwenye haki ya kucheza mashindano makubwa ni Azam, Yanga na Simba.
Lakini pia hii ni fursa kwao kujiuza sambamba na kuisaidia timu ya Taifa kupata wachezaji bora kwa sababu sasa hivi kila mmoja atapambana kwa kuwa anaamini inawezekana," alisema Pawasa.
Katika hatua ya nusu fainali, Stand United itavaana na Mtibwa Sugar na Singida United itawakabili JKT Tanzania baadaye.
Chanzo: Mwananchi
MaoniMaoni Yako