Chombo cha anga za juu cha China kimemeguka vipande vipande

Chombo cha anga za juu cha China kilichoacha kutumika Tiangong-1 kimemeguka vipande vingi kikiingia anga ya dunia na kuanguka maeneo ya bahari kusini mwa Pacific.
Chombo hicho kiliingia anga ya dunia saa 00:15 GMT Jumatatu, idara ya anga za juu ya China imetangaza.
Tiangong-1 ilirushwa angani mwaka 2011 kufanyia majaribio teknolojia ya kuunganisha vyombo mbalimbali anga za juu na pia vyombo vya kuzunguka kwenye mzingo wa dunia.
Chombo hicho ni sehemu ya juhudi za China za kuunda kituo cha anga za juu kitakachokuwa kinadhibitiwa na binadamu katika anga za juu kufikia mwaka 2022.
Kiliacha kufanya kazi Machi 2016.
Tunayoyafahamu kuhusu eneo ambalo kilianguka?
Maafisa wanasema tu kwamba kilianguka "juu ya Pacific Kusini".
Wataalamu wa anga za juu wa Marekani wamesema wametumia teknolojia ya kufuatilia mzingo wa dunia kuthibitisha kuingia ardhini kwa Tiangong-1.
Mtaalamu wa anga za juu Jonathan McDowell kutoka Harvard ameandika kwenye Twitter kwamba huenda chombo hicho kimeanguka kaskazini magharibi mwa Tahiti.
Kwanini chombo hiki kikaanguka hivi?
Tiangong kilifaa kusitisha shughuli yake ya kuizunguka dunia kwa utaratibu na mpangilio fulani.
Ni chombo kilichokuwa na urefu wa mita 10 (futi 32) na uzani wa zaidi ya tani 8 na ni kikubwa zaidi ya vyombo vyote vilivyoundwa na binadamu ambavyo vimewahi kuanguka kutoka anga za juu.
Lengo lilikuwa kutumia vifaa vinavyokipa chombo hicho msukumo kukielekeza hadi maeneo ya mbali yasiyo na watu maeneo ya Bahari ya Kusini.
Lakini kabla ya hilo kufanyika, ghafla mfumo wa kukidhibiti ulikumbwa na hitilafu na wataalamu wa China wakapoteza udhibiti.
Mashirika 13 ya anga za juu ya mataifa mbalimbali, yakiongozwa na Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA), yalifuatilia njia ya Tiangong na kujaribu kuiga tabia yake kadiri kilivyokaribia kuingia ndani ya anga ya dunia huku kikiendelea kuizunguka.
Source: BBC
MaoniMaoni Yako