Bushiri ataja sababu ya kupoteza dhidi ya SimbaKocha mkuu wa timu ya soka ya Njombe Mji Ally Bushiri amewapongeza wachezaji wake kwa kuonesha kandanda safi licha ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Mnyama Simba Sports Club katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara uliopigwa katika uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Bushiri amesema wachezaji wake walicheza vizuri na kwa umakini mkubwa lakini jambo pekee ambalo wenzao wa Simba waliwazidi hadi kupelekea kuruhusu mabao mawili ni kukosa uzoefu kama wachezaji wa Simba walivyokuwa.

"Wachezaji wa Simba wametumia uzoefu zaidi, kuweza kupata matokeo ya alama tatu katika mchezo huu, lakini ukweli mchezo ulikuwa na ushindani wa hali ya juu, vijana wangu wamejitahidi sana, ligi bado inaendelea, nadhani hata wewe umeshuhudia namna timu ilivyobadilika," Bushiri ambaye aliwahi kuionoa Mwadui amesema.

Tunawafadhaisha mashabiki

Kwa upande wa mlinda mlango namba ya moja wa Njombe Mji ambaye msimu uliopita alishuka daraja akiwa na timu ya Toto Africans ya Mwanza, David Kissu amesema wananjombe wasifadhaike na matokeo ya kufungwa na Simba kwani wao kama wachezaji wameumia na watajituma katika michezo ijayo ili kuwafuta machozi.

"Tunajua mashabiki wetu hawajafurahishwa na matokeo haya, wangependa kuona tunashinda katika mchezo huu hasa ukizingatia na nafasi ambayo tupo, lakini wasijali bado ligi inaendelea, niwahakikishie hatuwezi kushuka daraja ukiangalia mwenyewe table ilivyokaa ukishinda mechi mbili unatoka huku mkiani, tutapambana," Kissu amesema.

Kwa Njombe Mji huu unakuwa wa pili mfululizo kupata matokeo ya kufungwa katika michezo ya ligi, matokeo ambayo yanawafanya kuwa katika nafasi ya 15 wakiwa na alama 18 ambazo ni alama moja chini ya mstari salama wa kubaki kwenye ligi hiyo.
MaoniMaoni Yako