Azam wapata pigo BaraMABINGWA wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC,  watamkosa beki wake wa kimataifa, Daniel Amoah, ambaye atakuwa nje kwa muda wa miezi tisa kufuatia kuumia mguu, taarifa kutoka klabu hiyo, imeeleza
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa klabu hiyo, Jaffer Iddi, alisema taarifa kutoka kwa madaktari walioko Afrika Kusini zimeeleza kuwa mchezaji huyo atafanyiwa upasuaji mara mbili.
Iddi alisema kuwa baada ya kufika Afrika Kusini, ilibainika nyota huyo raia wa Ghana ana maumivu mengine ambayo nayo yalihitaji upasuaji ili aweze kurejea katika afya yake ya kawaida na hatimaye kucheza soka la ushindani.
"Leo (jana), alitarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kwanza, na atafanyiwa mwingine baadaye, taarifa ya daktari imesema atakaa nje kwa miezi tisa, hii inamaana kuwa atarejea uwanjani katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwakani," aliongeza Iddi.
Alisema pia kikosi chao sasa kitaelekeza nguvu zake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la FA na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
"Tumekubali matokeo, tumeondolewa katika Kombe la FA, sasa akili yetu iko katika Ligi Kuu, tunatarajia kwenda Mbeya Ijumaa tayari kwa mchezo dhidi ya Mbeya City ingawa tuna baadhi ya wachezaji majeruhi wa muda mrefu na mfupi," alisema kiongozi huyo.
Mbeya City itawakaribisha Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Chanzo: Ipp Media