Arsene Wenger: "Sijui kama nitakutana na Mourinho tena."Meneja wa Arsenal anayeondoka Arsene Wenger alisema hajui kama bado atakutana na meneja wa Manchester United Jose Mourinho tena baada ya timu yake kuchapwa 2-1 Jumapili.


Mechi hiyo ya Ligi ya Premia ilikuwa ya mwisho kwa Wenger dhidi ya mahasimu wao wa muda mrefu Manchester United akiwa kwenye usukani katika klabu ya Arsenal baada yake kutangaza majuzi kwamba ataondoka mwisho wa msimu.


United walitangulia kufunga dakika ya 16 Paul Pogba alipofunga bao lake la tatu katika mechi nne za karibuni ligini.


Henrikh Mkhitaryan aliwasawazishia Arsenal dakika ya 51 lakini Marouane Fellaini akafunga kwa kichwa zakika za mwisho mwisho na kuwapa United ushindi.


Wenger - ambaye timu yake ilishinda ligi uwanjani Old Trafford mwaka 2002 - alianza mechi hiyo akionekana mwenye tabasamu tele lakini akaondoka kwa masikitiko baada ya kuongezwa kwa mkimbio wa kutoondoka na ushindi Old Trafford hadi mechi 11 sasa.


Mfaransa huyo alikiri kwamba hana uhakika iwapo atakutana na Mourinho tena katika soka.


Alisema: "Yeye atakuwa Man Utd mwaka ujao bila shaka na sijui nitakuwa wapi wakati huo.


"Nimefanya kazi ya ukufunzi kiwango cha juu kwa miaka 35 mtawalia bila kupumzika na nafikiri kwa sasa mimi ndiye mtu pekee aliyefanya hivyo.


"Nipo katika eneo ambalo silifahamu vyema kusema kweli.


"Je, nitapumzika au nitaendelea na ukufunzi? Nijashangaa sana mwenyewe iwapo nitakutana naye mwaka ujao."


Wenger alikuwa ametania kabla ya mechi hiyo kwamba atakuwa daima anapokelewa vyema Old Trafford, akionekana kugusia uhasama wake wa muda mrefu na United.


Siku hiyo, haikuwa tofauti.


Mpinzani wake wa muda mrefu Sir Alex Ferguson alikuwa mfawidhi wa sherehe na kabla ya mechi alitoa zawadi kwa Mfaransa huyo.


Mashabiki walishangilia alipopewa bilauri ya fedha na meneja huyo wa zamani wa United.


Wawili hao walikumbatiana na kupigwa picha. Mourinho alijiunga nao kwa muda mfupi.


Wenger alipoulizwa baadaye kuhusu zawadi hiyo, alisema: "Sijui ni nini kilichomo. Sijaiangalia vyema. Ningependa kufurahia divai nyekundu na Sir Alex kwa sababu itakuwa ni divai nzuri. Unapoacha kuwa hatari tena, watu hukupenda."


Wenger alifanya mabadiliko manane kwenye kikosi chake, akionekana kuangazia zaidi mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Europa League Alhamisi ugenini Atletico Madrid, ambapo mechi ya kwanza walitoka sare 1-1.


Umri wa wastani wa kikosi chake ulikuwa miaka 24 na siku 67, kikosi changa zaidi cha Arsenal kuanza mechi ya Ligi ya Premia tangu Agosti 2011, wakati walipolazwa 8-2 uwanjani Old Trafford.


Arsenal wanasalia kuwa timu pekee kati ya zinazocheza ligi tano kuu England kutopata ushindi ugenini kufikia sasa mwaka 2018.


'Kumaliza nafasi ya pili'


United watapata nafasi ya mwisho ya kushinda kombe 19 Mei watakapokutana na Chelsea fainali ya Kombe la FA.


Ushindi dhidi ya Arsenal unawahakikishia nafasi ya kumaliza kwenye nne bora ligini na kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.


Lakini Mourinho amesisitiza kwamba wanataka kumaliza wa pili nyuma ya mabingwa Manchester City.


"Tulishinda alama tatu na hizo zinahitimisha mambo ya kuzufu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.


"Lakini bado tunahitaji alama nne kuhakikisha tunamaliza nafasi ya pili ambavyo tunataka."


United sasa wamo alama tano mbele ya Liverpool ambao wamo nafasi ya tatu. United hata hivyo wana mechi moja hawajacheza.


Masaibu ya WengerOld Trafford
Kando na uwanja wa Emirates na Highbury, Wenger ameshindwa mechi nyingi zaidi Old Trafford kama meneja wa Arsenal kuliko uwanja mwingine wowote ule.
United wamewashinda Gunners ligini nyumbani na ugenini msimu mmoja kwa mara ya kwanza tangu 2011-12.
Bao la Fellaini lilikuwa la kwanza kufungwa na United dakika ya 90 dhidi ya Arsenal Ligi ya Premia, na la kwanza kati ya timu hizo mbili tangu Januari 2007 Thierry Henry alipofunga Emirates na kuwapa Arsenal ushindi wa 2-1.
United wameshinda mechi zote 10 za Ligi ya Premia ambazo Pogba amefanikiwa kufunga.

fellain akishangilia goli lake dhidi ya Arsenal. 


Nini kinafuata?
Manchester United watakutana na Brighton Ligi ya Premia Ijumaa.
Arsenal nao watasafiri Uhispania kwa mechi ya marudiano Europa League dhidi ya Atletico Madrid Alhamisi. Watarejea ligini dhidi ya Burnley Jumapili.

Posted by Lebab
Chanzo: BBC

MaoniMaoni Yako