Yanga Wafanya Kikao Kizito


SAA chache kabla mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, kuondoka kwenda kambini mjini Morogoro, wachezaji na viongozi wa timu hiyo wamefanya kikao kizito kupanga mikakati ya namna watakavyoweza kuibuka na ushindi katika michezo inayowakabili.
Kikao hicho kilifanyika jana asubuhi katika makao makuu ya klabu hiyo Jangwani na kiliwahusisha wachezaji pamoja na viongozi wa Kamati ya Mashindano ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Hussein Nyika.
Akizungumza na SPOTI TZ mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema kikao hicho kililenga kuwakumbusha wachezaji majukumu yao uwanjani lakini pia kuwapa hamasa na kuwajenga kisaikolojia.
“Kama unavyojua hivi sasa Yanga imeyumba kiuchumi, hivyo viongozi wameona ni vyema kukaa na wachezaji kuwapa maneno machache kwa ajili ya kuwaongezea morali, lakini pia kuwapa hamasa na kuwajenga kisaikolojia ili wacheze kwa moyo wao wote,” alisema.
Alieleza kuwa uongozi wa klabu hiyo chini ya Katibu Mkuu wake, Charles Mkwasa na kamati ya mashindano, umeamua kufanya kikao hicho ili kutimiza malengo ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ambayo sasa wameingia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga waliangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa na Township Rollers ya nchini Botswana katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.
Hata hivyo, mjumbe huyo aliongeza kuwa Yanga pia inataka kutetea ubingwa wa Ligi Kuu msimu sambamba na kutwaa taji la Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup -ASFC).
Katika hatua nyingine, kikosi cha timu hiyo kiliondoka jana saa nane mchana kuelekea mji kasoro bahari, Morogoro, kuweka kambi ya siku tano kabla ya kuivaa Singida United mwishoni mwa wiki hii.
Yanga na Singida watachuana vikali katika mchezo wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho (FA) uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Namfua, Singida.
Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliliambia SPOTI TZ kuwa wachezaji wote wameondoka jijini Dar es Salaam kwenda Morogoro wakiwamo Donald Ngoma na Amiss Tambwe, isipokuwa Ibrahim Ajib, Hassan Kessy, Kelvin Yondani na Ramadhan Kabwili.
Nyota hao waliobaki walikuwa katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars’ ambacho jana kilicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) ambayo Taifa Stars iliibuka mshindi baada ya kuichalaza Timu ya Taifa ya Congo mabao 2:0, Wagingaji wakiwa Mbwana Samatta dakika ya '74 na Shiza Ramadhani Kichuya daklka ya '85 kabla yakutolewa.
“Tupo vizuri na wachezaji wote wapo fiti, leo wameingia kambini Morogoro lakini wale waliopo kwenye timu ya taifa wataungana na wenzao baada ya kumaliza majukumu yao,  kila kitu kipo poa,” alisema Hafidh.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Yanga kukutana na kikosi cha Singida kinachonolewa na kocha wao wa zamani, Mholanzi Hans van der Pluijm kwenye Uwanja wa Namfua, mechi ya kwanza ilikuwa ya Ligi Kuu na ilimalizika kwa sare ya bila kufungana
Chanzo:Bingwa
MaoniMaoni Yako