Simba SC wahaha kumbakiza Kichuya


  • ***Ni baada ya TP Mazembe na klabu nyingine kuonyesha nia ya kumsajili...
BAADA ya kuonyesha kiwango cha juu katika mechi ya kirafiki kati ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, anatakiwa na TP Mazembe, imefahamika.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinasema kuwa mabosi wa TP Mazembe wanajipanga kuja nchini kufanya mazungumzo na Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa ili kumsajili mchezaji huyo.
Mkataba wa Kichuya ambaye alitua Simba akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, rafiki wa karibu wa meneja wa Kichuya, Profesa Madundo Mtambo (jina tunalihifadhi) alisema kuwa umefika wakati wa mchezaji huyo kwenda kucheza soka la kulipwa akiwa bado ana umri mdogo na anauwezo wa kupambana kuzoea mazingira mbalimbali.
Chanzo hicho kilisema kuwa kwa sasa hawazingatii maslahi peke yake na wanachotaka kuona Kichuya anapata nafasi ya kubadili mazingira na kurejea tena nchini kuitumikia Taifa Stars akiwa na mbinu zaidi.
"Kwa sasa Profesa amesema wao hawaangalii fedha peke yake, wanaamini huu ni muda muafaka wa Kichuya kwenda kucheza Ulaya au nje ya Tanzania, na kwa sasa soko lake litakuwa rahisi kabla umri wake haujaongezeka zaidi," kilisema chanzo chetu.
"Maofisa wa Mazembe wanajiandaa kuwasiliana na timu ya Simba ya Tanzania kwa ajili ya kujadiliana kuhusu winga Shiza Kichuya," Obongosho amethibitisha, iliandika moja ya mitandao ya DRC.
SIMBA WANYWEAKaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah "Try Again" jana hakuwa tayari kusema lolote kuhusiana na mchakato wa mazungumzo ya kumsajili Kichuya yalipofikia.
Imeelezwa kuwa jana kiongozi huyo alifanya mawasiliano na Profesa Mtambo ili kuhakikisha wanapata saini ya winga huyo mwenye mabao saba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Chanzo: IPP Media
MaoniMaoni Yako