Niyonzima: nimerudi lakini sijafurahia


Kiungo wa kimataifa wa Simba, Haruna Niyonzima amerejea katika kikosi hicho baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kulikosababishwa na majeraha ya enka. 

Kiungo huyo wa kati alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu akitokea Yanga alikodumu kwa misimu sita mfululizo tangu msimu wa 2011/12 alipotokea katika timu ya APR ya Rwanda.
Aliichezea Yanga kwa mafanikio makubwa akiwa ni mchezaji wa kikosi cha kwanza kwa muda wote aliokuwa klabuni hapo. Championi Ijumaa limepata fursa ya kuzungumza na Niyonzima mara baada ya kuanza mazoezi yake ambapo ameelezea changamoto mbalimbali alizokutana nazo alipokuwa nje pamoja na mikakati aliyojiwekea katika kikosi chake hicho:

UNAENDELEAJE KWA SASA? 
“Matibabu yangu yalienda vizuri, nashukuru Mungu naendelea vizuri, natanguliza shukrani zangu kwa wale wote waliokuwa wakiniombea kipindi naumwa. “Siku zote utamtambua mwema wako ama mbaya wako pindi utakapokuwa unaumwa, nawashukuru watu wangu wote kwa sapoti yao walionipatia na kunifanya niwe fiti" Haruna alisema.

PROGRAMU ZAKO ZA MAZOEZI ZIPOJE? 
“Kwa sasa mwalimu amenipa programu maalumu ambazo nafanya kwa ajili ya kujiimarisha ikiwa ni pamoja na kukimbia kwa kuzunguka uwanja kisha nitaungana na wenzangu baadaye. Mwalimu ndiye anayejua wakati sahihi wa mimi kuanza kucheza mara baada ya kuniona nipo fiti, naamini nitakuwa sawa"
KWA SASA UPO FITI KWA KIWANGO GANI? “Bado sijakuwa fiti kama nilivyokuwa mwanzo, ndiyo narudi kidogo kidogo kwani nimetoka kwenye majeraha, nahitaji muda wa kujiweka fiti kwanza.
“Mara nyingi mashabiki wanapokuona uwanjani wanataka uonyeshe kiwango bila ya kufikiria hali yako ilivyo. Ikitokea mwalimu asiponitumia hadi msimu unaisha kwa upande wangu sitalaumu kwa kuwa yeye ndiye anayetambua ufiti wa mchezaji, natakiwa kuwa fiti ndipo anitumie".

UMEPEWA MASHARTI BAADA YA MATIBABU? 
“Awali niliporudi kutoka India kuna vitu nilitakiwa kuvifuatilia kabla ya kurejea uwanjani, ndiyo maana hata timu iliporejea sikuweza kujiunga nayo kutokana na maelekezo ya daktari wa India, lakini kwa sasa nimeshakamilisha ndiyo maana nimejiunga na timu.

UTARUDI INDIA KWA MATIBABU? 
“Hapana, matibabu niliyopewa yamejitosheleza na iwapo kutatokea kitu chochote kitakachonilazimu kurudi nitarudi.
VITU GANI ULIVIMISI ULIPOKUWA NJE YA UWANJA? “Nilimisi vitu vingi sana nilipokuwa nje ya kazi lakini nashukuru Mungu nimeweza kurudi kazini, hivyo najipanga kuitumikia timu yangu.

KIPI KILIKUUMIZA ULIPOKUWA NJE? 
“Niliumizwa jinsi baadhi ya watu walivyokuwa wakizungumza vitu mbalimbali juu yangu ambavyo havikuwa vya kweli. “Katika maisha yangu sikuwahi kukaa nje kwa muda mrefu kama ilivyokuwa hivi sasa, nimepitia katika wakati mgumu, watu wanatakiwa watambue, mpira ndiyo kazi ninayoitegemea katika maisha yangu, ninasomesha na kuendesha vitu mbalimbali ambavyo siwezi kuvitaja kwa kutegemea mpira. “Hivyo, siwezi kudharau kazi yangu, mtu anatoka kusikojulikana na kuanza kunizungumzia mimi vitu tofauti, watu hawanitembelei kuangalia hali yangu wala, kuna Watanzania wamekuwa wazuri wa kuongea kuliko vitendo.

WANASIMBA WATARAJIE NINI KUELEKEA LALA SALAMA YA VPL? “Hii si kwa Niyonzima pekee, tunatakiwa tujiandae kisaikolojia, kujiweka fiti ili tuweze kufanya vizuri mechi zote kumi zilizosalia. Iwapo hatutofanya vizuri na kushindwa kutwaa ubingwa msimu huu, itakuwa jambo baya kwani tutashindwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, hivyo tunahitaji kupambana.
“Wanasimba wajue mimi sijarufahia kuwa nje, na hakuna ambaye ana mkataba na maradhi lakini nia yangu ni kuisaidia Simba, lakini kwa sasa hata kama ninakuwa nje ya uwanja, napenda kuona timu yangu ikifanya vizuri.
UNAIZUNGUMZIAJE LIGI? “Ligi kwa jumla ni ngumu ina ushindani mkubwa kila timu imejipanga kupata matokeo mazuri, hivyo ni vyema tukaliona hilo ili kuweza kufanya vyema.

YANGA KUWA NAFASI YA PILI HAKUKUTISHI?
“Hiyo ni hamasa kwetu wachezaji kwa kuwa tunajua kuna mtu anatufuata kwa nyuma, tukizubaa tumekwisha, tunajua ili tushiriki kimataifa msimu ujao lazima tuchukue ubingwa wa ligi, pia hata wachezaji tunakuwa na hamasa ya kupambana. “Pia wakumbuke kuwa katika ligi Simba haijafungwa hadi sasa, hilo ni jambo zuri na la kupongezwa, sisi hatuangalii zaidi Yanga japo ni changamoto kwetu na kila mchezaji anaseti akili yake kuwa hatutakiwi kupoteza. “Hata kama mimi sipo uwanjani, tuna umoja wa wachezaji na benchi la ufundi. Kila mechi sasa kwetu ni fainali.”

Source : Champion
Na: Agape Patrick
Email: agape m@spoti.co.tz

MaoniMaoni Yako