Niyonzima nae bado wiki aanze kusakata


Siku chache baada ya kurejea uwanjani na kuanza mazoezi mepesi, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima raia wa Rwanda, amepewa zaidi ya wiki moja ya kuwa sawa kabisa kabla ya kuanza rasmi kucheza mechi zijazo ikiwemo ile dhidi ya watani wao wa jadi Yanga.
Niyonzima aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mguu, hivi karibuni alianza mazoezi mepesi jambo ambalo limelifanya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mfaransa, Pierre Lechantre kufurahia urejeo wake.
Mbali na Niyonzima kurejea, lakini pia beki wa timu hiyo, Salim Mbonde, naye ameanza mazoezi sambamba na Niyonzima baada ya kutoka kwenye majeraha ya goti, kisha kupata ajali hali ambayo ilimfanya akae nje ya uwanja tangu Oktoba, mwaka jana.
Endapo wawili hao wakiwa fiti kwa muda huo waliopewa, basi wataweza kucheza dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao unatarajiwa kupigwa Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.
Akiwazungumzia wachezaji wake hao, Lechantre alisema kurejea kwao kikosini, kunamfanya akione kikosi chake ni kipana zaidi, lakini kwa sasa ni mapema kuanza kuwatumia kwenye mechi, hivyo anawapa zaidi ya wiki moja kuwa fiti.
“Nimefurahi kuwaona wamereja katika kipindi hiki ambacho tunapambana kuhakikisha tunamaliza ligi salama.
“Niyonzima na Mbonde nawapa wiki moja zaidi ya kuwaangalia kama watakuwa fiti ili nianze kuwatumia, sina haraka nao, nataka wakirudi uwanjani wawe tayari kwa kucheza na kuipambania timu,” alisema Lechantre ambaye ndiye kocha pekee Mfaransa kwenye Ligi ya Bongo kwasasa.
Tayari kuna wiki nne kabla ya mechi ya Simba na Yanga ambayo inaaminika kuwa wachezaji hao watakuwa fiti kabisa kuicheza.

Na: Pgape Patrick
Email: agape@spoti.co.tz
Source: Saleh Jembe
MaoniMaoni Yako