KAGAME CUP KUPIGWA DAR JUNI MWAKA HUU


Michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati inayosimamiwa na Baraza la vyama vya soka ukanda huo (CECAFA) maarufu kama Kagame Cup yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwezi Juni mwaka huu.

Michuano hiyo inarejea baada ya kupita miaka mitatu kufuatia kukosena kwa wadhamini huku bingwa mtetezi akiwa Azam FC.

CECAFA imepokea kiasi cha dola Milioni moja kutoka Shirikisho la soka duniani (FIFA) ili kufanikisha mashindano mbalimbali yakiwemo ya vijana chini ya umri wa 17 yatakayofanyika nchini Burundi, pamoja yale ya Wanawake na Wanaume kwa nchi wanachama.

Taarifa za ndani kutoka katika uongozi wa CECAFA zinasema kuwa michuano hiyo itafanyika kati ya Juni 30 hadi Julai 14 jijini Dar badala ya Djibouti kama ilivyotangazwa awali.

Taarifa zimezidi kusema kuwa michuano hiyo ilipangwa kufanyika nchini Djibouti lakini Azam TV ambao wameingia mkataba kurusha matangazo hayo moja kwa moja wameshauri kubadilishwa kutokana na sababu za kiusalama.

Simba ndio inaongoza kwa kutwaa taji hilo mara nyingi ikifanya hivyo mara sita ikifuatiwa na Yanga na Gor Mahia zilizotwaa mara tano.
Source: Sports Kitaa


MaoniMaoni Yako