Tuesday, July 7, 2020

Simba yajichimbia Mtwara kuzivutia kasi Namungo, Yanga

Simba yajichimbia Mtwara kuzivutia kasi Namungo, Yanga
Baada ya mchezo wa dhidi ya Ndanda jana kikosi chetu kimeendelea kubaki mkoani Mtwara kwa ajili kujiandaa na mechi mbili muhimu dhidi ya Namungo siku ya Jumatano na ile ya nusu fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup itakayopigwa Jumapili dhidi ya Yanga.

Kocha mkuu, Sven Vandenbroeck amesema mechi zote mbili muhimu na tunapaswa kushinda ili kuudhihirisha umma kuwa tumestahili kuwa mabingwa wa nchi kwa mara ya tatu mfululizo.

Sven amesema kikosi kimebaki Mtwara na kitaendelea na mazoezi kwa vipindi viwili kwa siku asubuhi na jioni kikijiwinda na mechi hizo mbili ambazo tunapaswa kupata matokeo ya ushindi.

"Kikosi kitaendelea kubaki hapa kujiandaa na mechi yetu ya Jumatano dhidi ya Namungo na ile ya Jumapili ya FA. Zote ni mechi muhimu kikubwa tunahitaji kucheza vizuri na kupata ushindi," amesema Sven.

Kocha Sven amesema baada ya mchezo dhidi ya Numungo kikosi kitarejea tena Mtwara na asubuhi ya siku itakayofuata kitasafiri hadi jijini Dar es Salaam.

Baada ya mchezo dhidi ya Namungo tutakabidhiwa taji letu la ubingwa wa ligi msimu wa 2019/20 ambalo tumelitwaa tukiweka historia ya kuwa na mechi sita mkononi.

Simba, Ndanda zagawana pointi Nangwanda

Simba, Ndanda zagawana pointi Nangwanda
Simba, Ndanda zagawana pointi Nangwanda
Mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba SC dhidi ya Ndanda SC uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona umemalizika kwa sare ya bila kufungana huku timu zote zikigawana vipindi katika kufanya vizuri. Simba ilikuwa bora zaidi kipindi cha kwanza ikifanya mashambulizi mengi langoni mwa Ndanda lakini walikuwa imara kuhakikisha hawaruhusu magoli wakionekana kuhitaji hata alama moja kutokana na nafasi waliopo kwenye msimamo. Kipindi cha pili Ndanda nao walirudi kwa kasi na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Simba lakini hata hivyo idara yetu ya ulinzi ilikuwa imara kuhakikisha hairuhusu kufungwa.
Simba wakipokea gwaride la heshima kutoka kwa Ndanda FC kabla ya kuanza mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara

Kipindi cha pili kocha Sven Vandenbroeck alifanya mabadiliko ya kuwatoa Pascal Wawa, Luis Miquissone, John Bocco na Gerson Fraga nafasi zao zikachukuliwa na Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Meddie Kagere na Said Ndemla lakini hata hivyo hawakuweza kubadili ubao wa matokeo. Baada ya matokeo ya leo tumefikisha pointi 80 ambazo zinaendelea kuimarisha ubingwa wetu ambao ni wa kihistoria kutokana na kutwaa tukiwa tumesaliwa na mechi sita mkononi. Mchezo unaofuata utakuwa dhidi ya Namungo utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi siku ya Jumatano na baada ya mechi tutakabidhiwa taji letu la ubingwa.

Kanda ndani leo kuivaa Ndanda

Kanda ndani leo kuivaa Ndanda

Winga Deo Kanda amepangwa katika kikosi cha kwanza kwenye mchezo dhidi ya Ndanda SC utakaopigwa katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara saa 10 jioni.

Kocha Sven Vandenbroeck amesema ameamua kumuanzisha Kanda ili kuimarisha safu ya ushambuliaji kuimaliza Ndanda ukizingatia kwamba winga huyo amekuwa nje kwa muda mrefu baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Yanga 

Kabla ya kuumia Kanda alikuwa kwenye kiwango bora  ambapo baada ya kupata maumivu kabla ya ligi kusimama kupisha mlipuko wa homa ya virusi vya corona Kanda amekuwa akitumika kama mchezaji wa akiba au kucheza katika mechi za kirafiki.

Mlinzi Kennedy Juma ambaye alishindwa kuendelea na mchezo wa robo fainali ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Azam FC tulioshinda mabao 2-0 leo ameanza tena kwenye kikosi hatua inayoonyesha yuko fiti.

Baada ya kuonyesha viwango bora kwenye michezo uliopita ukiwemo dhidi ya Azam nahodha wetu John Bocco, Luis Miquissone na Clatous Chama wataongoza safu ya ushambuliaji.

Kikosi kamili kinachoivaa Ndanda SC

1. Aishi Manula
2. Haruna Shamte
3. Gadiel Michael
4. Kennedy Juma
5. Pascal Wawa
6. Jonas Mkude
7. Deo Kanda
8. Gerson Fraga
9. John Bocco ©
10. Clatous Chama
11. Luis Miquissone


Wachezaji wa Akiba
Gk. Ally Salim 
2. Said Hamis
3. Erasto Nyoni 
4. Mzamiru Yassin
5. Hassan Dilunga
6. Medie Kagere 
7. Francis Kahata

Ni mechi ya Heshima leo hapa Nangwanda

Kikosi chetu leo kinashuka dimbani kuikabili Ndanda SC katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Ndanda SC utakaofanyika uwanja wa Nangwanda Sijaona ambao utakuwa ni wakuweka heshima kwa upande wetu. Wiki iliyopita tulitawazwa mabingwa wa ligi kuu baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons hivyo mechi zetu zote sita zilizobaki zitakuwa zakuweka heshima. Ukiacha kutwaa ubingwa wa mara ya tatu mfululizo Simba tumeweka historia ya kutwaa taji huku tukiwa na mechi sita mkononi kitu ambacho hakijawahi kutokea hapo kabla. Kocha mkuu, Sven Vandenbroeck amesema licha yakuwa tayari tumetwaa ubingwa lakini atahakikisha tunashinda mechi zote zilizobaki kuweka heshima. "Tayari tumechukua ubingwa wa ligi lakini hatuwezi kubweteka tumejipanga kuhakikisha tunaweka heshima kwa kushinda mechi zote zilizobaki. Kuwa na idadi kubwa ya pointi kutatufanya kuweka historia kwa klabu," amesema Sven. TAKWIMU BAINA YETU KILA TUNAPOKUTANA Katika michezo nane ambayo tumekutana na Ndanda tumeshinda saba na kutoka sare mmoja. Licha yakuwa tunapata ushindi dhidi ya Ndanda lakini mara zote wamekuwa wakitupa ushindani mkubwa. Matokeo ya mechi tano zilizopita kati ya nane tulizokutana na Ndanda Simba 2-0 Ndanda Simba 2-0 Ndanda Ndanda 0-0 Simba Ndanda 0-2 Simba SImba 3-1 Ndanda TAARIFA YA TIMU Meneja wa timu Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wote 27 waliosafiri wako tayari kwa mchezo hivyo benchi la ufundi litakuwa na wigo mpana kupanga kikosi. Rweyemamu amesema tutaingia kwenye mchezo wa leo kwa kuiheshimu Ndanda ingawa haipo katika nafasi nzuri kwenye ligi.

PICHA: Simba yapiga 'mazoezi' ya mwisho kabla ya kuivaa Ndanda Kesho

PICHA: Simba yapiga 'mazoezi' ya mwisho kabla ya kuivaa Ndanda Kesho
Kikosi jioni ya leo kimefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Nangwanda Sijaona kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa ligi utakaopigwa kesho dhidi ya Ndanda SC saa 10 jioni. Meneja Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wote 27 waliosafiri wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo hivyo benchi la ufundi litakuwa na wigo mpana wa kupanga kikosi. Mapema mchana wa leo kocha mkuu, Sven Vandenbroeck amesema baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi tunataka kumaliza kwa heshima kwa kushinda mechi zote zilizobaki tukianza na wa kesho dhidi ya Ndanda.
Sharaf Eldin Shiboub akifanya mazoezi na wenzake kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda FC

Aishi Manula (kushoto) na Jonas Mkude wakifanya mazoezi kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda FC

Gerson Fraga akipiga tizi Uwanja wa Nangwanda Sijaona tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda FC

Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda FC

Said Ndemla akifanya mazoezi leo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda FC

Sven: Baada ya ubingwa tunataka kumaliza ligi kwa heshima

Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amesema sasa kikosi chake cha Simba SC kinajipanga kuhakikisha tunamaliza ligi kwa heshima kwa kuendelea kupata alama tatu katika kila mchezo baada ya kutawazwa mabingwa wa ligi kuu msimu wa 2019/20.

Kuelekea mchezo wa kesho wa ligi dhidi ya Ndanda utakaopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Sven amesema mchezo utakuwa mgumu ukichangiwa na ubovu wa sehemu ya kuchezea ya dimba hilo.

Sven amesema baada ya timu kuwa katika wakati mzuri kwenye mchezo uliopita wa robo fainali ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Azam FC tulioibuka  na ushindi wa mabao 2-0 anaamini mechi ya kesho haitakuwa na kasi ile kutokana na uwanja.

Raia huyo wa Ubelgiji amesema baada ya kukagua uwanja hasa eneo la kuchezea amegundua mchezo utakuwa mgumu lakini amewaandaa wachezaji kukabiliana na hali hiyo.

"Tumetangazwa mabingwa tayari lakini haitufanyi tusizipe umuhimu mechi zilizobaki. Tumejipanga kuhakikisha tunamaliza ligi kwa heshima kwa kushinda kila mchezo uliobaki.

"Mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda utakuwa mgumu na utachangiwa na uwanja kutokana na eneo la kuchezea si zuri sana lakini tumejiandaa kuhakikisha tunakabiliana na hali hii ili kupata alama tatu," amesema Kocha Sven.

Kikosi chawasili salama Mtwara, Kapombe, Rashid wabaki Dar

Kikosi chetu kimewasili salama mkoani Mtwara kikiwa na wachezaji 27 tayari kwa mechi mbili za ligi dhidi ya Ndanda FC keshokutwa Jumapili na Namungo itakayochezwa Julai 8. Nyota wetu wawili mlinzi Shomari Kapombe na winga Rashid Juma wamebaki jijini Dar es Salaam kutokana nakuwa majeruhi hivyo wanaendelea na matibabu. Kapombe ameumia goti katika mchezo wetu uliopita wa robo fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup tulioibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC baada ya kuchezewa rafu na Frank Domayo.
Sharaf Eldin Shiboub

Kiungo Sharaf Eldin Shiboub ambaye alitua mapema wiki hii nae ni miongoni mwa wachezaji waliopo hapa Mtwara baada ya kuchelewa kurejea kutoka nchini kwao Sudan kutokana na mipaka kufungwa sababu ya mlipuko wa virusi vya ho Corona. Meneja wa timu, Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wote waliosafiri wapo kwenye hali nzuri na wamejiandaa kutoa burudani katika mechi zote mbili. "Kikosi kimewasili salama hapa Mtwara kikiwa na wachezaji 27 na tumejiandaa kutoa burudani kwa mashabiki wetu katika mechi zote mbili. Kapombe na Rashid wao wamebaki Dar es Salaam kwasababu ni majeruhi," amesema Rweyemamu.
Kiungo Clatous Chama akishangiliwa na umati mkubwa wa mashabiki wa Simba waliojitokeza kupokea timu ilipowasili Mtwara

Winga Luis Miquissone akishingaliwa na mashabiki wa Simba waliojitokeza kupokea timu mkoani Mtwara

Simba yaifuata Ndanda Mtwara, kukabidhiwa ubingwa Ruangwa

Kikosi cha Simba kimeondoka leo asubuhi kuelekea mkoani Mtwara kwa ajili ya mchezo wa ligi dhidi ya Ndanda FC utakaopigwa kesho kutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Baada ya mchezo kikosi kitaelekea Ruangwa mkoani Lindi kucheza na Namungo ambapo tutakabidhiwa ubingwa wa ligi msimu 2019/20.

Meneja wa Timu, Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mechi hizo mbili ambazo lengo ni kuhakikisha tunachukua pointi zote sita.

"Kikosi kimeondoka leo asubuhi kuelekea Mtwara tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Ndanda na kisha tutacheza na Namungo huku tukitarajia kutakabidhiwa taji la ubingwa mkoani Lindi," amesema Rweyemamu.

Sherehe na shamra shamra za ubingwa zitafanyika katika Uwanja wa Majaliwa baada ya mchezo wetu dhidi ya Namungo ambapo tutakabidhiwa taji letu.

Dk. Gembe: Tusubiri vipimo hatma ya Kapombe

Daktari wa timu, Yassin Gembe amesema mlinzi wa kulia Shomari Kapombe ambaye alipata majeraha katika mchezo wa jana dhidi ya Azam FC amefanyiwa vipimo katika Hospitali ya Hitech Sai Health Care iliopo Upanga majibu yake yatatoka kesho.

Kapombe aliumizwa na kiungo Frank Domayo dakika ya mwisho ya mchezo ambapo leo amepelekwa hospitali ili kujua ukubwa wa jeraha na matibabu yake yatachukua muda gani.

Dk. Gembe amewataka wapenzi na mshabiki wa Simba kuwa na subira mpaka kesho ili kuweza kufahamu ukubwa wa jeraha la mlinzi huyu mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kwa ufasaha nafasi nyingi uwanjani.

"Kapombe amefanyiwa vipimo leo na kesho tutapata majibu yake kuwa ameumia kwa kiasi gani na matibabu yake yatachukua muda gani," amesema Dk. Gembe.

Kapombe ndiye aliyesaidia kupatikana kwa bao la pili (kutoa assist) lililofungwa na Clatous Chama dakika ya 56 kwenye ushindi wa 2-0 tulio upata dhidi ya Azam.

SportPesa yaimwagia Simba mamilioni ya ubingwa

Mdhamini mkuu wa klabu yetu Kampuni ya SportPesa leo imetoa hundi ya kiasi cha milioni 100 kama bonasi baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu wa 2019/20.

Fedha hizo ni sehemu ya mkataba tuliosaini nao mwaka 2017 ambapo kila tutakapofanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi tutapokea kiasi hicho cha fedha.

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas ameipongeza Simba kwa kupeperusha vema nembo ya kampuni yao kama wadhamini wetu wakuu kwa kuendelea kufanya vizuri na kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya tatu mfululizo.

"Leo tunaikabidhi hundi ya Shilingi milioni 100 kama bonus baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi msimu 2019/20 kama tulivyokubaliana kwenye mkataba tuliosaini mwaka 2017.

"Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi, uongozi na mashabiki kwa mshikamano wenu hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa huu tena kwa mara ya tatu mfululizo," amesema Tarimba.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ameipongeza SportPesa kwa kuendelea kuinua soka la Tanzania ambapo anafurahi kuendelea kufanya kazi na kampuni hii.

"Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi nchini ya Mwenyekiti Mohammed Dewji tunaishukuru SportPesa kwa kutimiza vigezo vya mkataba na tunaahidi kuendelea kufanya vizuri ili kuitangaza nembo yao," amesema Senzo.

Sven akunwa na kiwango cha wachezaji mechi na Azam

Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wetu katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup uliopigwa uwanja wa Taifa jana.

Kocha Sven amesema kikosi kilitawala dakika zote 90 za mchezo na kila mchezaji alijitoa kuhakikisha tunapata matokeo na hata waliokuwa benchi walikuwa na morali ingawa hawakupata nafasi.

Sven amesema anaamini kiwango kilichoonyeshwa kwenye mchezo wa jana kitaendelea hivyo hadi mwisho wa msimu ambapo sasa tunaelekeza nguvu katika mechi mbili zijazo dhidi ya Ndanda na Namungo.

"Nimefurahishwa na kiwango cha wachezaji wangu walichoonyesha. Kila mmoja alitimiza majukumu yake vilivyo na hata wale ambao hawakupata nafasi walikuwa wapo tayari kuisaidia timu. Tulitawala dakika zote 90," amesema kocha Sven.

Akizungumzia madhambi aliyofanyiwa mlinzi wetu Shomari Kapombe kocha Sven amesema lilikuwa tukio baya na anaamini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litachukua hatua stahiki.

"Kama mchezaji wetu Jonas Mkude alifungiwa mechi mbili kwa kufanya madhambi basi naamini hata kwa aliyemfanyia Kapombe naye atachukuliwa hatua stahiki," amesema kocha Sven.

Kapombe aliumizwa goti la mguu wa kulia kiungo Frank Domayo dakika za mwisho za mchezo tukio ambalo mwamuzi hakuliona.

Simba yaichakaza Azam, yatinga nusu fainali FA

Simba yaichakaza Azam, yatinga nusu fainali FA
Simba SC leo imefanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa.

Ukiachana na matokeo hayo ambayo yametupeleka nusu fainali kikosi chetu kimeonyesha uwezo mkubwa wa kutandaza kabumbu ambalo limewavutia mashabiki ambapo kilitawala mchezo muda wote.

Nahodha John Bocco alitufungia bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 39 baada ya kupokea mpira wa krosi uliopigwa na Francis Kahata.

Mlinzi wetu Kennedy Juma alishindwa kuendelea na mchezo dakika ya 41 baada ya kukanyagwa na Obray Chirwa nafasi ikachukuliwa na Erasto Nyoni.

Clatous Chama alitupatia bao la pili kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango Benedict Haule baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Shomari Kapombe.

Dakika 10 za mwisho za kipindi cha pili wachezaji wetu waliamua kumiliki mpira kwa kupiga pasi kitu ambacho kiliwafanya mashabiki kulipuka kwa furaha.

Mchezo wa leo ni wa nne msimu huu kukutana na Azam ambapo tumefanikiwa kushinda mechi zote.

Baada ya kuitupa nje Azam sasa tutakutana na watani wetu Yanga katika hatua ya nusu fainali.

Sunday, June 28, 2020

Kikosi cha Simba dhidi ya TAnzania Prisons Leo
Kagere, Hajibu kuongoza mashambulizi dhidi ya Prisons leo


Mshambuliaji kinara Medie Kagere na fundi wa mipira ya mwisho Ibrahim Hajibu wamepangwa kuongoza mashambulizi katika mchezo wetu wa leo dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigiwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa. Katika michezo miwili iliyopita kocha Sven Vandenbroeck amemtumia nahodha John Bocco kama mshambuliaji pekee huku mara zote Kagere akitokea benchi. Kagere ambaye ndiye kinara wa ufungaji akiwa na mabao 19 kwenye ligi amepangwa kuongoza mashambulizi katika mchezo muhimu ambao tunahitaji sare pekee ili kutwaa ubingwa. Kwa upande wa Hajibu hakupata nafasi kubwa ya kucheza katika mechi mbili zilizotangulia tangu kurejea kwa ligi lakini amekuwa kwenye kiwango bora anapocheza mechi za kirafiki na amekuwa akifunga kila mchezo. Mlinzi wa kulia Haruna Shamte naye ameanza kuchukua namba ya Shomari Kapombe ambaye amekuwa akitumika mara zote kama ilivyo kwa Gadiel Michael aliyechukua nafasi ya Mohammed Hussein upande wa kushoto. Mzamiru Yassin anaanza kwenye mchezo wa leo akichukua nafasi ya Said Ndemla ambaye ametengeneza maelewano mazuri na Gerson Fraga katika eneo la kiungo cha ulinzi kwenye mechi mbili zilizopita. Kikosi Kamili kilivyopangwa
Kikosi Kamili kilivyopangwa
1. Aishi Manula
2. Haruna Shamte
3. Gadiel Michael
 4. Erasto Nyoni
 5. Kennedy Juma
6. Gerson Fraga
 7. Hassan Dilunga
 8. Mzamiru Yassin
 9. Medie Kagere
10. Ibrahim Hajibu
11. Miraji Athumani

WACHEZAJI WA AKIBA Gk. Ally Salim 12. Mohamed Hussein 13. Pascal Wawa 14. Said Hamis 15. Clatous Chama 16. John Bocco 17. Luis Miquissone

Pointi moja tu Sokoine tutwae taji VPL 2019/20

empty:news-banner-img

Pointi moja tu Sokoine tutwae taji VPL 2019/20Ni dhahiri sasa Simba SC inakaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom 2019/20 ambapo inahitaji pointi moja pekee kumaliza shughuli hiyo.


Simba sasa iko jijini Mbeya ikisubiri mechi ya leo dhidi ya Prisons ikihitaji pointi hiyo moja tu ambapo tayari imeshacheza na Mbeya City Jumatano na kuifunga mabao 2-0. Iwapo katika mchezo wa leo Simba ikipata sare itafikisha pointi 79 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote Leo tukifanikiwa kutwaa ubingwa tutakuwa tumechukua kwa mara ya tatu mfululizo. KAULI YA KOCHA SVEN KUELEKEA MECHI YA LEO Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amesema atatumia mfumo wa mipira mirefu kama alivyofanya kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City kutokana na Uwanja wa Sokoine kutoruhusu kucheza soka la pasi fupi. "Tutatumia mipira mirefu kama tulivyofanya katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, hatutacheza soka la pasi za chini kama kawaida yetu kwakua hali ya uwanja haituruhusu kufanya hivyo," amesema Kocha Sven. Kuhusu hali ya kikosi kocha Sven amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na wapo tayari kwa mchezo ambao amekiri utakuwa mgumu. MKUDE KUENDELEA KUBAKI JUKWAANI Kiungo Jonas Mkude ataukosa mchezo kama ilivyokuwa mechi iliyopita kutokana na kuendelea kutumikia adhabu ya kukosa michezo miwili ambayo inakamilika leo. Matokeo ya mechi tano zilizopita dhidi ya Prisons Simba 0 - 0 Prisons Prisons 0 - 1 Simba Simba 1 - 0 Prisons Simba 3 - 0 Prisons Prisons 2 - 1 Simba

Simba kuingia na mbinu za Mbeya City kuimaliza Prisons kesho

empty:news-banner-img

Simba kuingia na mbinu za Mbeya City kuimaliza Prisons keshoKocha Mkuu, Sven Vandenbroeck ameweka hadharani mbinu atakazotumia katika mchezo wa kesho dhidi ya Prisons kuwa ni kama alizotumia katika mchezo dhidi ya Mbeya City Jumatano wiki hii.


Katika mechi hiyo, Sven alitumia mipira ya juu kutokana na Uwanja wa Sokoine kutoruhusu soka la pasi fupi ambalo tumelizoea kutokana na eneo lake la kuchezea (pitch) kutokuwa zuri. "Tutatumia mipira mirefu kama tulivyofanya katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, hatutacheza soka la pasi za chini kama kawaida yetu kwa kuwa hali ya uwanja haituruhusu kufanya hivyo," amesema Kocha Sven. Simba imekuwa ikisifika kwa soka safi la pasi za haraka za chini lakini Kocha Sven ameamua kubadili mfumo huo ili kuendana na hali ya Uwanja. Licha ya kuweka wazi kuwa atatumia mfumo wa mipira mirefu kocha Sven ameahidi kucheza soka safi la kuvutia kama ilivyo kawaida ya timu yetu. Kuhusu hali ya kikosi kocha Sven amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na wapo tayari kwa mchezo isipokuwa kiungo Jonas Mkude ambaye anamalizia adhabu yake ya kufungiwa mechi mbili. "Wachezaji wote wako vizuri wana ari tayari kwa mchezo wa kesho, isipokuwa tutaendelea kumkosa Mkude ambaye anamalizia adhabu yake ya kukosa mechi mbili," amesema kocha Sven

PICHA: Simba yapiga 'tizi' Sokoine kuivutia kasi Prisons Jumapili

empty:news-banner-img

PICHA: Simba yapiga 'tizi' Sokoine kuivutia kasi Prisons JumapiliKikosi leo asubuhi kimefanya mazoezi katika uwanja wa Sokoine tayari kwa maandalizi ya mchezo wa ligi siku ya Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons.


Jana kikosi kilifanya mazoezi ya utimamu wa mwili kwa wachezaji ambao walicheza mechi dhidi ya Mbeya City ambapo leo wamefanya kwa pamoja. Wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri ambapo tutaendelea kukosa huduma ya kiungo Jonas Mkude ambaye amefungiwa mechi mbili na hii ya Prisons itakuwa ya mwisho.

Ibrahim Ajib akifanya mazoezi na wachezaji wenzake leo asubuhi Juni 26 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya


Said Ndemla akifanya mazoezi na wachezaji wenzake leo asubuhi Juni 26 katika Uwanja wa Sokoine


Clatous Chama (kushoto) na Said Ndemla wakiwania mpira katika mazoezi yaliyofanyika leo asubuhi Juni 26 katika Uwanja wa Sokoine


Pascal Wawa (kulia) na Meddie Kagere wakifanya mazoezi leo asubuhi Juni 26 ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons


Clatous Chama akifanya mazoezi leo Juni 26 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya

Fraga: Nitaendelea kufanya vizuri kila nikipangwa

empty:news-banner-img

Fraga: Nitaendelea kufanya vizuri kila nikipangwa

Kiungo mkabaji raia wa Brazil, Gerson Fraga ameahidi kuendelea kufanya vizuri katika kila

dakika atakayoipata atakapokuwa anaitumikia timu hii.

Fraga amekuwa katika kiwango bora kufuatia kupata nafasi ya kucheza katika michezo miwili iliyopita ya ligi dhidi ya Mwadui na Mbeya City baada ya kurejea kwa ligi. Fraga amesema anafurahishwa na jinsi mashabiki wanavyotoa ushirikiano kwake pamoja na timu nzima ndio maana wanajitahidi kuhakikisha katika kila mchezo wanawapa furaha Wanasimba. "Mimi kama mchezaji kazi yangu ni kuhakikisha naisaidia timu kushinda kila mchezo ambao nitapata nafasi ya kucheza. Lengo langu nikuisaidia Simba kutwaa ubingwa na kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika mwakani," amesema Fraga. Fraga amewataka mashabiki kuendelea kuisapoti timu popote walipo katika michezo iliyosalia jambo ambalo litawaongezea hamasa kwao kupigania timu kupata ushindi. Nawaomba mashabiki wetu kuendelea kutusapoti katika mechi yetu iliyobaki ili tufanikishe kuchukua ubingwa," amesema Fraga.

Matola awavulia kofia mashabiki Mbeya

empty:news-banner-img

Matola awavulia kofia mashabiki Mbeya

Kocha Msaidizi wa Timu ya Simba, Suleiman Matola amewasifu mashabiki waliojitokeza kwa

wingi kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City jana katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Matola amesema mashabiki hao walikuwa chachu kubwa ya ushindi wa mabao 2-0 tuliyopata kwani wachezaji walikuwa wakijiona wana deni muda wote. Pamoja na hayo, Matola pia amewataka mashabiki hao kujitokeza tena kwa wingi katika mchezo ujao wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa katika uwanja huo huo wa Sokoine ili tupate ushindi na hatimaye tutawazwe mabingwa. "Nimefurahishwa na wingi mashabiki waliojitokeza jana, mchango wao ulikuwa mkubwa na tunawaomba waje tena kwenye mchezo wetu dhidi ya Prisons Jumapili," amesema Matola. Kwa upande wake nahodha John Bocco amesema ushindi wa jana unatokana na ushirikiano mkubwa baina ya wachezaji ndani ya uwanja benchi la ufundi na mashabiki. "Ushindi huu unatokana na ushirikiano mkubwa baina ya wachezaji ndani ya uwanja kila mmoja wetu lengo lake ni kupata ushindi," amesema Bocco.

Wednesday, June 24, 2020

Bocco aingamiza Mbeya City akitupia mbili

empty:news-banner-img

Bocco aingamiza Mbeya City akitupia mbili

Mabao mawili yaliyofungwa na Nahodha John Bocco 'Adebayor' yametosha kutupa ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Bocco alitufungia bao la kwanza dakika ya tano ya mchezo baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Clatous Chama akiwa ndani ya 18. Baada ya bao hilo Mbeya City waliongeza kasi ya kutaka kusawazisha kwa kufanya mashambulizi mengi lakini safu yetu ya ulinzi iliyokuwa chini ya Pascal Wawa na Kennedy Juma ilikuwa imara. Dakika ya 54 Bocco tena aliipatia timu bao la pili kwa 'kuchop' akimalizia pasi iliyopigwa kwa ufundi mkubwa na Francis Kahata na kumuacha mlinda mlango wa City, Aaron Kalambo akiwa hana la kufanya. Dakika ya tatu ya nyongeza kipindi cha pili mwamuzi Athumani Lazi alikataa bao lililofungwa na Miraji Athumani akitafsiri kulikuwa na madhambi ingawa marejeo ya video yameonyesha hakukuwa na faulo. Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck, alifanya mabadiliko ya kuwatoa Kahata na Said Ndemla nafasi zao zikachukuliwa na Luis Miquissone na Mzamiru Yassin. Matokeo haya yanatufanya kufikisha pointi 78 baada ya michezo 31, ambapo sasa tunahitaji alama tano ili tutangazwe mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo.

Chama, Miraji ndani ya nyumba dhidi ya Mbeya City Leo

empty:news-banner-img

Chama, Miraji ndani ya nyumba dhidi ya Mbeya City Leo

Viungo washambuliaji Clatous Chama na Miraji Athumani leo wataanza katika mchezo wa ligi kwa mara ya kwanza tangu iliporejea baada ya mapumziko ya ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona.
Chama alichelewa kujiunga na wenzake baada ya kwenda nchini kwao Zambia hivyo kukosa mazoezi ya mwanzoni wakati Miraji ametoka kwenye majeruhi ya muda mrefu hivyo mechi ya leo dhidi ya Mbeya City itakuwa ya kwanza kwa wao kuanza. Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting, Chama hakucheza wakati Miraji aliingia kutokea benchi na mechi ya pili dhidi ya Mwadui Chama alitokea benchi huku Miraji akiwa hajacheza. Kwa mara nyingine kocha Sven Vandenbroeck amewaanzisha Said Ndemla na Gerson Fraga katika eneo la kiungo wa ulinzi ambao mchezo uliopita dhidi ya Mwadui walifanya vizuri. Nahodha John Bocco ameanza tena kama mshambuliaji kiongozi kama ilivyokuwa katika mechi iliyopita akisaidiwa na Francis Kahata, Miraji na Chama. Kikosi kamili kitakachoshuka dimbani ni: 1. Aishi Manula 2. Shomari Kapombe 3. Mohamed Hussein 4. Kennedy Juma 5. Pascal Wawa 6. Gerson Fraga 7. Said Juma 8. Clatous Chama 9. John Bocco (c) 10. Miraji Athumani 11. Francis Kahata Wachezaji wa Akiba Gk. Ally Salim 2. Mzamiru Yassin 3. Gadiel Michael 4. Erasto Nyoni 5. Medie Kagere 6. Ibrahim Hajibu 7. Luis Miquissone

Simba Kamili kuivaa Mbeya City Leo Sokoine

empty:news-banner-img

Simba Kamili kuivaa Mbeya City Leo Sokoine


Kikosi chetu leo kitashuka katika uwanja wa Sokoine jijini hapa kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City kikiwa kamili tayari kwa kuzisaka pointi tatu. Tunaingia kwenye mtanange huu tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 4-0 tuliopata kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza. Mchezo huo ambao ulipigwa Novemba 3 mwaka jana katika uwanja wa Uhuru mabao yetu yalifungwa na Medie Kagere kwa mkwaju wa penati, Clatous Chama, Sharaf Eldin Shiboub na Deo Kanda. KAULI YA KOCHA SVEN Kuelekea mchezo wa leo kocha, Sven Vandenbroeck amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja yupo tayari ingawa amekiri mechi itakuwa ngumu. "Wachezaji wote wapo vizuri kimwili na kiakili, tunategemea kupata ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani ukizingatia watakuwa nyumbani lakini lengo letu ni lile lile pointi tatu," amesema kocha Sven. NAHODHA NAE ATOA NENO Nahodha wa timu John Bocco 'Adebayor' amesema wanafahamu mchezo utakuwa mgumu lakini lengo la kwanza itakuwa kuhakikisha tunapata pointi zote tatu. "Tunafahamu mechi itakuwa ngumu kwakua kila timu inahitaji pointi tatu katika kipindi hiki ligi ikielekea ukingoni lakini sisi tumejipanga kukabiliana chochote kitachotokea ili kupata pointi tatu," amesema Bocco. Matokeo ya mechi saba zilizopita kati yetu na City Simba 4-0 Mbeya City Mbeya City 1-2 Simba Simba 2-0 Mbeya City Simba 2-2 Mbeya City Mbeya City 0-2 Simba Simba 2-0 Mbeya City Mbeya City 0-1 Simba

Matola awahakikishia furaha Wanasimba kesho

empty:news-banner-img

Matola awahakikishia furaha Wanasimba kesho

Kocha Msaidizi, Suleiman Matola amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi katika mechi mbili ndani ya Jiji la Mbeya huku akiwahakikishia furaha kwani ana uhakika wa kupata ushindi.
Kikosi cha Simba kesho kitashuka katika Uwanja wa Sokoine kuikabili Mbeya City na Jumapili kitarejea dimbani hapo kumenyana na Tanzania Prisons. Matola amesema hali ya hewa ya jiji la Mbeya ni baridi kali lakini wachezaji wapo kwenye hali nzuri na wana ari kitu kinachomfanya kuamini katika kupata ushindi kwenye mechi hizo mbili. Nahodha huyo wa zamani wa Simba amesisitiza mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kutoa sapoti kwa wachezaji. "Hali ya hewa ya Mbeya ni baridi sana, tumeanza mazoezi tangu jana kwa awamu moja, wachezaji wako vizuri tayari kwa mapambano. "Tunawaomba Wanasimba watusapoti kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani tunachowaahidi ni kuwa hatutawaangusha kutokana na jinsi wachezaji walivyo tutahakikisha lazima tupate matokeo ya ushindi tukianza na mchezo wa kesho dhidi ya City," amesema Matola.

Kauli ya Bocco kabla ya kuzifuata City na Prisons Mbeya

empty:news-banner-img

Kauli ya Bocco kabla ya kuzifuata City na Prisons Mbeya

Nahodha wa Timu ya Simba, John Bocco amesema wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na alama zote sita katika michezo miwili dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Bocco amesema hayo kabla ya kuondoka alfajiri leo Jumatatu Juni 22, kuelekea jijini Mbeya huku akiweka wazi kuwa wachezaji wana ari na kila mmoja anahitaji ushindi kwenye mechi hizo. Bocco amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika michezo hiyo ili kuwatia nguvu na hatimaye kwa pamoja lengo la kupatikana kwa pointi sita lifanikiwe. "Mpaka muda huu tunaondoka wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na lengo la kila mmoja ni kupata alama zote sita katika michezo miwili. "Tunafahamu mechi zitakuwa ngumu kwa kuwa kila timu inahitaji pointi tatu katika kipindi hiki ligi ikielekea ukingoni lakini sisi tumejipanga kukabiliana na chochote kitachotokea ili kupata pointi zote," amesema Bocco. Jumatano wiki hii kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Sokoine kuikabili Mbeya City na mwishoni mwa wiki tutacheza na Prisons zote za jijini Mbeya.

Sunday, June 21, 2020

Simba yajipima kwa kuipiga 'mkono' Lyon

Simba yajipima kwa kuipiga 'mkono' Lyon


Simba yajipima kwa kuipiga 'mkono' Lyon

Simba yajipima kwa kuipiga 'mkono' Lyon
Kikosi chetu kimeibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa kirafiki uliopigwa leo Jumapili Juni 21, katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Katika mechi hiyo kama kawaida yake Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck aliwatumia wachezaji ambao hawakuanza au kucheza kwenye mchezo wa jana dhidi ya Mwadui FC ambao tuliibuka na ushindi wa mabao 3-0. Simba ilipata mabao manne ndani ya dakika saba kuanzia dakika ya 25 hadi ya 32 yaliyofungwa na wachezaji Ibrahim Ajibu aliyefunga mawili, Tairone Do Santos kwa mkwaju wa penati na Mzamiru Yassin. Winga Deo Kanda aliyetokea benchi alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la mwisho dakika ya 87. Utaratibu wa mechi za kirafiki baada ya mechi ya ligi uliwekwa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck mahsusi kwa ajili ya wachezaji ambao wanakuwa hawajatumika kucheza siku inayofuata ili kuwafanya kuwa fiti. Baada ya ligi kusimama takribani miezi mitatu na wachezaji kutofanya mazoezi ya pamoja Kocha Sven amesema anaamini ili warudi katika ushindani wa kweli wanapaswa kupata muda mwingi wa kucheza uwanjani. Kikosi kilichoanza kilikuwa hivi: Ally Salim, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Yusuf Mlipili, Tairone Do Santos, Mzamiru Yassin Francis Kahata, Clatous Chama, Medie Kagere, Ibrahim Ajib na Miraji Athumani Baadae kocha alifanya mabadiliko ya kuwaingiza Rashid Juma, Cyprian Kipenye, Kanda na Shiza Kichuya kuchukua nafasi za Kagere, Mlipili, Shamte na Kahata.

Huu ndio ujumbe wa kocha Sven kwa wachezaji

Huu ndio ujumbe wa kocha Sven kwa wachezaji

 Ally Shatry Sat, Jun 20th 2020
Licha ya kuwapongeza kwa kucheza vizuri katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC kocha mkuu, Sven Vandenbroeck amewataka wachezaji wake waendelee kujituma katika mechi zinazofuata ili watangaze ubingwa mapema. Ujumbe huo unatokana na ratiba yetu ilivyo kwakua mwanzoni mwa mwezi ujao tutakuwa na mchezo mgumu wa robo fainali ya michuano ya FA dhidi ya Azam FC ambapo Sven anataka mpaka muda huo tuwe tumetawazwa mabingwa. Kocha Sven amesema amefurahi kuona wachezaji wake wakishika mafunzo ya kubadili mfumo wa uchezaji kwa haraka ndani ya siku tatu na kuutumia vema uliopelekea kupatikana kwa ushindi huu mnono. "Ujumbe wangu kwa wachezaji ni kuwataka kuendelea kujituma, kujitoa kwa ajili ya timu ili tutangaze ubingwa mapema. Tutakuwa na ratiba ngumu kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao," amesema kocha Sven. Kwa upande wake kocha msaidizi, Suleiman Matola amewapongeza wachezaji kwa kucheza vizuri huku akiwataka wafanye hivyo katika mechi zijazo dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City. "Nichukue nafasi kuwapongeza wachezaji kwa kucheza vizuri na kufanikiwa kupata ushindi mnono, kikubwa nawataka wasibwete twende Mbeya tukafanye kama tulichofanya kwa Mwadui," amesema Matola.

Simba yalipa Kisasi kwa Mwadui Taifa na kutandaza soka safi

Simba yalipa Kisasi kwa Mwadui Taifa na kutandaza soka safi
empty:news-banner-img

Simba yalipa Kisasi kwa Mwadui Taifa na kutandaza soka safi


Mchezo wetu wa ligi kuu dhidi ya Mwadui FC uliopigwa uwanja wa Taifa umemalizika kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku tukionyesha kandanda safi la kuvutia. Mechi hii ilikuwa ni ya kisasi kutokana na mzunguko wa kwanza Mwadui kutufunga kwa bao moja katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga hivyo tulipaswa kuhakikisha tunachukua pointi zote tatu. Kiungo mshambuliaji Hassan Dilunga ndiye aliyetufungulia karamu ya mabao kwa kufunga la kwanza dakika ya nane baada ya kazi nzuri iliyofanywa na nahodha John Bocco. Mlinzi Augustino Samson alijifunga na kutupatia bao la pili dakika ya 21 katika jitihada za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe ndani ya kisanduku cha sita. Bocco alitufungia bao la tatu dakika ya 57 kufuatia shuti kali lililopigwa na Luis Miquissone kugonga mwamba wa juu na mpira ukamkuta nahodha ambaye aliumalizia kwa kichwa. Kocha Sven Vandenbroeck aliwatoa Bocco, Dilunga, Miquissone, Kapombe na Gerson Fraga na kuwaingiza Clatous Chama, Medie Kagere, Francis Kahata, Yusuph Mlipili na Mzamiru Yassin ambao nao waliendelea kucheza soka safi lililowavutia mashabiki. Ushindi huu umetufanya kufikisha pointi 75 tukiendelea kuongoza kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 30.