Senzo: Tulieni muone balaa Usajili Yanga

1 month ago 211

YANGA wamesahau kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Simba na habari iliyo mbele yao sasa ni usajili mpya.

Senzo Mazingiza ambaye ni mshauri wa uongozi wa Yanga amesema ndani ya wiki mbili kuanzia jana watakuwa wamekamilisha.

Amesema wamejidhatiti na Yanga ijayo itakuwa imara zaidi na yenye uwezo wa kupambana Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Septemba 11. Senzo amesema jana walikuwa na kikao viongozi wote kuhakikisha wanakamilisha usajili wa wachezaji na kuwarejesha kambini mapema.

“Tuna muda mfupi sana na tunatakiwa tukamilishe usajili wa wachezaji wapya haraka kwenye kikosi chetu na tukikutana ndio tutajua,” amesema Senzo na kuongeza Alhamisi hii wataanza kucheza na anga kushusha vifaa.

Amesema watakuwa makini upande wa usajili wa ndani na nje, huku nje umakini ukiwa mkubwa zaidi kutokana na msimu ujao wapo kwenye mashindano ya kimataifa. “Tunatakiwa tukamilishe usajili wa Caf kabla ya tarehe 15 (mwezi ujao) kwa hiyo tuna kazi ya kufanya na tupo makini, wiki hii mpaka ijayo tutakuwa tumekamilisha asilimia kubwa usajili wote.”

Baada ya kutua Dar viongozi wote walipanda taksi na kuongozana kwenda ofisi za timu hiyo kuendeleza mipango ya usajili msimu ujao.

“Kweli hatujapata kombe la Ligi wala FA msimu huu, lakini tunaenda hatua kwa hatua, wachezaji wetu wamepambana kuhakikisha tunachukua kombe ila haijawa hivyo, msimu ujao naamini tutachukua makombe kulingana na usajili tutakaoufanya,” alisema.

“Mchezo wetu wa fainali dhidi ya Simba tayari matokeo yameshatokea tumepoteza, kadi nyekundu imetuyumbisha kwa namna fulani lakini tushasahau matokeo hayo kwa sasa.”

Naye kipa Faruk Shikhalo alisema: “Kadi nyekundu ilichangia kupoteza mchezo, Simba hawakuwa bora zaidi.”