Miquissone athibitisha kutimkia Al Ahly kwa Bilioni 2

1 month ago 247

Miquissone  athibitisha kutimkia  Al Ahly kwa Bilioni 2

Baada ya kurudi kazini uongozi wa Simba, uliokuwa bize kwa ajili ya fainali kombe la Shirikisho (ASFC) na kubeba taji hilo mbele ya Yanga wamekutana na email iliyotoka Al Ahly ambayo imeeleza kumuhitaji Luis Miquissone.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya Simba, mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly wanamtaka Miquissone na wapo tayari kutoa kitita cha Dola za Kimarekani milioni 2, ambayo kwa pesa ya Kibonge ni zaidi ya Sh4 Bilioni.

Taarifa hiyo inaeleza Al Ahly wamevutiwa na Miquissone kutokana na sababu nne za msingi, kwanza kipaji chake cha kucheza soka, umri wake anaweza kucheza muda mrefu au kuuzwa katika timu nyingine zaidi ya pesa hiyo ambayo wataitoa.

Sababu mbili za mwisho ni ubora alionyesha katika mechi ya Al Ahly iliyochezwa Uwanja wa Mkapa pamoja na kufunga bao kali na sababu ya nne kocha, Pitso amekuwa akivutiwa zaidi ya Nyota huyo ambaye aliwahi kuwa nae Afrika Kusini.

Baada ya hayo yote Bodi ya Wakurugenzi Simba, itakutana ikiwemo kumshirikisha kocha, Didier Gomes ili kufanya maamuzi ya kwamba watamuachia Miquissone kwani mkwanja ambao walikuwa wanahitaji ili kumuuza Al Ahly wameufikia.

Mmoja wa watu wa ndani ya Simba, alisema Al Ahly wanamtaka kweli Miquissone na wameamua kutoa kiasi hicho kikubwa cha pesa ili kukamilisha dili hiyo bila ya kuwepo kizui kuhusu masuala ya kimaslahi.

ADVERTISEMENT

“Sasa kazi imebaki kwa Simba wenyewe kama watafanya maamuzi ya kuachana na Miquissone au wataamua kubaki nae kutokana na mahitaji ya kufanya vizuri zaidi katika mashindano hayo ya kimataifa msimu ujao,” alisema.

Awali Mwanaspoti lilikujuza Uongozi  wa Simba ulikuwa kama umeshalifahamu jambo hilo siku nyingi na walianza harakati za kumtafuta mbadala wa Miquissone na kura zilimdondokea, Mzambia Moses Phiri.

Wakati Simba wakiamini Phiri anaweza kuwa mbadala wa Miquissone inaelezwa Gomes, amewambia bado staa huyo wa Zambia hataweza kuziba pengo lake kwahiyo waingie zaidi sokoni kumtafuta mwingine.

Mwanaspoti lilimtafuta Miquissone ambaye alisema mchezaji yoyote ambaye anafanya vizuri katika wakati fulani lazima atahusishwa kusajiliwa na timu nyingine inaweza kuwa ndani ya nchi au nje.

Miquissone alisema jambo hilo ndio anakutana nalo wakati huu ila hizo timu ambazo zimekuwa zikimuhitaji zinatakiwa kwanza kufika kwa Uongozi wa Simba kwani bado yupo na mkataba na waajili wake.

“Mnafahamu kila kitu kuhusu usajili wangu na Simba, bado nipo na mkataba nao kwahiyo kama kuna timu nyingine zinanihitaji wanatakiwa kwanza kuanzia huko na baada ya hapo ndio nitapatiwa taarifa zao na viongozi wangu,” alisema Miquissone ambaye bao lake aliliwafunga Al Ahly linaweza kuwa bao bora la mashindano hayo msimu huu.

“Ambacho nafahamu timu zipo nyingi si hapa ndani ya Afrika bali hata Ulaya nimekuwa nikiona mawakala wengi ambao wote nawapeleka kwa uongozi,” alisema Miquissone ambaye bado anamkataba wa mwaka mmoja na nusu na Simba.