UNAPOEPUKA MITEGO YA MWANAMKE USIYE NA NIA NAYE

Sunday, 22 April 2012

MWANAMKE USIYE NA NIA NAYEMWANAMUME asiye na mpenzi huwa na wakati mgumu anapokuwa katika pilika za kumtafuta mwanamke wa kuwa naye, ambaye anaweza kumfaa kuwa mkewe baadaye. Tatizo si kwamba wanawake hawapatikani, bali ni kwamba bila kujua, anaweza kujikuta ameukwaa mkenge kwa kumpata mwanamke ambaye hakuwa katika akili yake, hivyo kuathiri mustakabali mzima wa maisha yake.

Huko duniani wapo wanawake wanaojidhania kuwa wamepuuzika kiasi cha kutosha na kwamba sasa wanataka wenza. Huyu ukimwingia kwa majaribio atakuganda kama ruba na unaweza ukajikuta ukimvalisha pete bila hata kufahamu. Katika hali hii, hata pendekezo dogo tu la kutaka mtoke jioni kwa ajili ya matembezi linaweza kuwa njia ya kukunasa. Kama umempenda hakuna tatizo, lakini kama bado uko katika utaratibu wa kusafisha macho na kupima kabla hujaamua uchukue kitu kipi, ni wazi kuwa utajikuta katika wakati mgumu.
Si kwamba wasichana wote huwang’ang’ania wanaume ili wawaoe. Lakini unapaswa kuwa makini na kila mwanamke unayezungumza naye na pengine kumtania kuhusiana na maisha ya baadaye ya unyumba. Namna pekee ya kuwa salama na mikono ya wanawake wenye kupenda kuwaganda wanaume ni kuepuka mambo fulani fulani ambayo baadhi yamebainishwa hapa chini.
Mambo mengine yanaweza kuonekana mazuri na yenye nia njema, lakini kama hutakuwa makini, na pengine kama hujakamilisha masuala muhimu ya maisha yako, utashangaa unaitwa baba fulani na utake usitake utawajibika kwa matokeo ya kazi yako.
1. MATEMBEZI
Ni jambo la kawaida kuwaona wenza wakitembea barabarani, wakiwa wameshikana mikono, pengine wakiwa wamejikita katika mazungumzo ya kina. Kwa hao hakuna tatizo, maana tayari wako pamoja. Lakini kwako wewe ambaye bado unapepesapepesa macho, mwanamke anaweza kulitumia jambo hilo kama njia yake ya kukuteka.
Kama bado huna uhakika na mwanamke huyu na huna mpango wa kumfuatilia, usikubali kufuatana naye katika matembezi ya aina hii maana atakupitisha miongoni mwa watu na kukutambulisha (japo anaweza asiseme neno), ilimradi ajenge mazingira ya kuufanya umma uamini kuwa mko pamoja.
Mbali na kwamba matembezi yenu yanaweza kuishia katika nyumba ya kulala wageni, lakini pia kwa kuuonesha umma mnaokutana nao njiani kuwa mko pamoja, anarahisisha kazi yake ya kukuvuta maishani mwake, maana tayari zitaanza kuibuka tetesi mitaani kuwa mnapendana. Kama ulikuwa huna habari, basi tambua kuwa matembezi ni jambo la kimahaba. Kumbuka jambo lolote la kimahaba unapaswa kumfanyia mwanamke ambaye unamjali, ambaye hakika unamhitaji maishani mwako na si yule ambaye ulijisemesha kwa utani kuwa unampenda na akakusikia.
2. MWALIKO
Mwanamke mwenye malengo makubwa na wewe atakualika kujumuika naye katika hafla mbalimbali na atapenda pia kukualika katika kampani ya marafiki zake, wa kike na wa kiume. Anaweza pia kukukaribisha katika eneo ambako huenda kufanya mazoezi, au mahali ambapo huenda kupata burudani, mathalani michezo. Kitakachofuata hapo, ni kukufanya kuwa sehemu ya maisha yake na usipokuwa makini utajikuta ukiwa mpenzi wake, bila hata kutumia dawa yoyote.
Linaweza kuwa jambo dogo tu. Pengine mnasoma pamoja na baada ya masomo anakualika kwenye mgahawa fulani wa wazi kwa ajili ya kupata kahawa au soda. Baada ya hapo anaweza kupendekeza mwe mnajisomea pamoja wikiendi na baadaye utajikuta mwenyewe ukijaribiwa kufanya jambo jingine na yeye. Taratibu unaweza kujikuta ukiwa mpenzi wake.
Hutakiwi kuepuka moja kwa moja kufanya jambo lolote na msichana unayeweza kumtongoza, lakini hakikisha kuwa unakuwa makini na kuidhibiti hali yoyote itakayojitokeza kama huna mpango na msichana huyo. Ni suala la kuwa wazi. Mwoneshe msimamo wako uko wapi na hata kama atakasirika lakini atakuelewa. Tena ni vema akikuelewa, maana atatambua kuwa hupendi kupoteza naye muda wako, kwani pengine unaye mlengwa mwingine.
3. KUKUPIKIA CHAKULA
Wapo wanawake wanaodhani na kuamini kuwa njia rahisi zaidi ya kumpata mwanamume ni kupitia katika tumbo lake. Jambo hili linaweza lisiwe kweli kwa wanaume wote lakini lina chembe za ukweli. Mwanamke huufahamu udhaifu wa mwanamume katika kupenda vyakula vizuri na kwa sababu hii atakualika kwake na kukukaangizia, ili akuoneshe jinsi utakavyofaidi kama utaamua kuwa naye kama mke.
Lakini unapokuwa kwake, pia utakuwa chini ya himaya yake na si rahisi sana kufurukuta kwa lolote, maana umejipeleka mwenyewe. Lakini zaidi, kitendo cha kukupikia atakichukulia kuwa cha kimahaba na usipokuwa makini chakula chake kitalipa. Vilevile, utakapobaini kuwa ameingia gharama kwa ajili ya kukukirimu, utajiwa na huruma za kibinadamu na hivyo kujisemea moyoni kuwa unahitaji kulipa fadhila, hivyo kama hutakuwa makini, utapendekeza aje kwako au mtoke mwende viwanja ili ulipe fadhila.
Katika hali hii, haihitajiki shahada ya saikolojia kubaini kuwa utakuwa unaelekea mikononi mwake, maana kwa kiasi fulani tayari amekuteka. Na kwa kuwa safari moja huanzisha nyingine, yamkini mtafurahia siku hiyo na kupanga kukutana siku nyingine, maana mmeshazoeana.
Kama utataka kumpiku, mwalike nyumbani kwako na umpikie. Kwa kuwa utakuwa kwako, mambo yote yatakwenda kama unavyotaka wewe, maana wewe ndiwe umeshika hatamu. La muhimu unapomwalika kwako ni kuhakikisha kuwa una kifua cha kuvumilia, maana anaweza kukufanyia vituko. Hakikisha tu kwamba unakuwa mbali na kitanda chako huku ukiwa umeazimia kuwa kama mambo yatakuwa mabaya utamwonesha mlango atoke aende zake salama. Kama unahisi kuwa anaweza kutaka kung’ang’ania kwako, haifai kumwalika. Hakikisha tu kwamba mambo yenu yanaishia nje, tena ikibidi kwenye hadhara.
4. FILAMU
Kwenda kuangalia filamu mahala ni jambo la kawaida na si lazima uende na mpenzi wako au mpenzi wako mtarajiwa. Lakini zipo filamu ambazo hazifai kuangalia na mwanamke asiyekuwa wako, kwani huamsha mihemko ya kimapenzi. Kuna uwezekano kuwa ukiwa naye hatapendelea kuangalia filamu za vita wala za ngono, lakini angalau atataka kuangalia filamu zenye matukio ya maisha, mapenzi na mahaba.
Kama huna mpango wowote wa baadaye na mwanamke, hakikisha kuwa humkubalii pendekezo lake la kuangalia filamu za mahaba. Akiziangalia filamu hizo atapata hisia za hali ya juu na kwa kuwa utakuwa naye atakusumbua. Kwa sababu hiyo, ni vema kuangalia filamu za kawaida, pengine makala ya maisha ya wanyamapori, sanaa za maonesho na kadhalika, lakini si mapenzi na mahaba.
5. MARAFIKI ZAKE
Wakati fulani mwanamke anaweza kukupigia simu na kusema: “Mimi na marafiki zangu tutakuwa pahala fulani kwa ajili ya kinywaji, waweza kuungana nasi?” Ni mwanamume gani mwenye ujasiri wa kukataa ofa nzuri kama hii? Ni yule tu mwenye uwezo wa kunusa mitego ya mwanamke.
Ukishajiingiza katika mtandao wa marafiki zake unaweza kujikuta ukiwa mhanga wa penzi lake. Pengine unaweza ukabahatisha, marafiki zake wakawa hawakukupenda, wakaona unawawekea kiwingu maana ukiwapo hawazungumzi mambo yao. Lakini unaweza kujikuta mtu mwenyewe kumbe ni mchangamfu na mcheshi, wakakupenda na kuwashinikiza wewe na yule aliyekuita mfanye kweli. Unaweza ukawa huvutiwi naye lakini ukaanza kumpenda kutokana na shinikizo.
Kama utataka kwenda, watafute wapambe kadhaa uende nao. Hawa watakusaidia kuvuruga mipango yoyote ya mwanamke ya kukuteka na pengine mmoja wao anaweza kumhitaji na akamchukua. Lakini ukienda mwenyewe kichwakichwa utaanguka mtegoni.
KUWA MAKINI
Unapokutana na msichana ambaye unahisi moyo wako unampenda, hutafikiria jambo jingine zaidi ya kuwa naye viwanja na kujirusha naye. Ni jambo ambalo kijana yeyote wa kiume atalipenda. Lakini si hivyo kwa msichana ambaye hajakuvutia, ambaye huna mpango naye, kwani huyu badala ya kufurahia kampani yake utaona kana kwamba anakuwekea kiwingu. Kama hujafikiria kuishi na mwanamke au hata kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi, ni vema kuzingatia mambo yaliyobainishwa hapo juu ili kuweza kuikwepa mitego ya wanawake wajanja.
Si kila msichana atakayetaka ushirikiane naye katika mambo yaliyobainishwa hapo juu atakuwa na ajenda yake, hapana. Wapo wasichana ambao watakupenda na kuipenda kampani yako lakini katika muktadha wa urafiki wa kawaida na unaweza ukakuta tayari anaye wake. La muhimu zaidi ni kuwa makini usije ukaishia kujuta kwa kuangukia pabaya. Maisha ya ujana ni mazuri, si busara kuyaharibu kwa kuingia katika unyumba na mwanamke ambaye hakuwa chaguo lako. Kumbuka majuto ni mjukuu.

MWANAMUME asiye na mpenzi huwa na wakati mgumu anapokuwa katika pilika za kumtafuta mwanamke wa kuwa naye, ambaye anaweza kumfaa kuwa mkewe baadaye. Tatizo si kwamba wanawake hawapatikani, bali ni kwamba bila kujua, anaweza kujikuta ameukwaa mkenge kwa kumpata mwanamke ambaye hakuwa katika akili yake, hivyo kuathiri mustakabali mzima wa maisha yake.
Soma zaidi

SIFA MUHIMU ZA KUZINGATIA UTAFUTAPO MTU WA KUISHI NAYE

Tuesday, 10 April 2012

MARA nyingi vijana hupata taabu sana katika suala la kuchagua mchumba. Vijana wa kiume ndio hasa hupata wakati mgumu zaidi kwani jamii imewapa wajibu wa kuanzisha mazungumzo yahusianayo na mapenzi. Hata hivyo, vijana wa kike nao wanao wajibu wa kuchagua ili kuhakikisha kuwa hawaanguki mikononi mwa mabazazi wa kuwalaghai na kuwatumia kwa raha za miili yao kisha kuwaacha kwenye mataa.

Ni jambo la kawaida kwa vijana walio wengi, wawe wa kike au wa kiume, kuangalia sura na mwonekano wa mtu. Lakini unapotafuta mchum
Soma zaidi

Parachichi, itasaidia mno kulainisha ngozi yako

Friday, 23 March 2012

ParachichiVITU vya asili navyo vinasaidia kuweka ngozi kuwa nzuri wakati wowote ule, ngozi ni kiungo kikubwa kwa binadamu hivyo inatakiwa kuwa waangalifu kuitunza ili kuepusha isizurike na kitu kingine chochote.

Ngozi ni kiungo ambacho kinachopokea magojwa haraka hivyo ndio maana tunaambiwa ni vizuri kuitunza ili isipoteza uasilia wake.

Ngozi nzuri ni ile ambayo haijapoteza uasilia wake wakati wote na kila siku uonekana vilevile ilivyo lakini hiyo inatokana na jinsi mtu anavyoweza kuitunza ngozi hiyo.

Kwa upande wa wanawake tunathamini mno ngozi ya usoni tofauti na sehemu nyingine katika mwili,  kwani ngozi ya uso ni muhimu na vilevile ni rahisi kushika vigonjwa vidogovidogo ambavyo vinavyokuwa vinaharibu ngozi yako.
Soma zaidi

JINSI YA KUWAKUNA WAZAZI WA MKEO MTARAJIWA

Friday, 23 March 2012

PENGINE tayari umempata msichana ambaye unamwita mpenzi wako au mchumba wako, umempenda naye ameonekana kukupenda na tayari ameishakukutanisha na marafiki zake. Hata hivyo, bado hujafanikiwa kukutana na wazazi wake.

Katika hali ya kawaida ni kwamba kama huyo mpenzi wako ana wazazi na anaelewana nao vizuri, lazima tu atakutambulisha kwao, ama kama mchumba, au rafiki. Katika tamaduni za kimagharibi, msichana humtambulisha pia boyfriend wake kwa wazazi na ndugu
Soma zaidi

Jinsi ya kukabiliana na makwazo ya awali ya mwanamke

Thursday, 15 March 2012

KWA mtu ambaye ndiyo kwanza anajiingiza katika ulimwengu wa mapenzi, ni dhahiri kuwa atakutana na mambo mengi ya kumkwaza, ambayo hatimaye yanaweza kumvunja moyo kuhusiana na suala zima la mapenzi. Wanaume, hususan kwa kuwa ndio wenye jukumu la kuanzisha mahusiano, hujikuta katika wakati mgumu wanapokwenda kukabiliana na wanawake, kutokana na tabia za wanawake, hasa wasichana za kutaka kujilinda.
Wanaume wengi wamekata tamaa na kubaki wakinung'unika, kutokana na kusalimu amri kwa makwazo mbalimbali yatokanayo na tabia ya asili ya mwanamke, ya kumjaribu mwanaume.
Mojawapo ya makwazo ambayo huweza kumkuta mwanaume katika uwanja wa mapenzi ni maswali ya 'kijinga' ambayo mwanamke anaweza kumuuliza, kwa ajili ya kuangalia msimamo wake.
Japo yameitwa ya 'kijinga' lakini maswali haya yana mchango mkubwa katika mapenzi, kwani majibu yatolewayo na mwanamume kwa maswali haya ni muhimu katika mustakabali wa mapenzi. Pamoja na hayo, wapo wanaume ambao hulalamika kuwa wameshindwa kuwaelewa wanawake, hususan kuelewa maana ya yale wayazungumzayo, yakiwamo maswali yao.
Mathalani, unaweza kuwa umepanga miadi na mwanamke kwa ajili ya kutoka naye, lakini saa mbili kabla ya muda mliopanga kutoka anakwambia kuwa ameahirisha suala hilo mpaka siku nyingine, tena anakupa ujumbe huo kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, au hata ujumbe wa sauti, badala ya kupiga simu au kukutana nawe ana kwa ana.
Kana kwamba hiyo haitoshi, unapoonekana kufadhaika mwanamke huyo huyo anaweza kukuuliza, "Kwani vipi, mbona hivi? Una nini leo? Unaonekana uko mbali kabisa kimawazo. Uko sawa lakini?" Hii inaweza kuwa saa kadhaa baada ya kuitolea nje ofa yako ya kutoka ambayo aliishaikubali awali.
Wakati mwingine unaweza kuwa umetoka naye mara kadhaa, lakini mara hii unapomwambia suala la kutoka anakuuliza "Lakini uhusiano wetu huu unaelekea wapi? Si tunapoteza muda tu lakini?"
Maswali ya aina ya kwanza hapo juu yanaonekana ni ya kijinga, kwa sababu mwanamke huyu anafahamu fika kuwa mabadiliko ya hisia zako yametokana na hatua yake ya kuahirisha mtoko katika dakika za majeruhi.
Vivyo hivyo, maswali ya aina ya kwanza yanaweza kuitwa ya kijinga, kwani mwanamke angeweza kusubiri na kuelezwa umepanga kwenda wapi na si kukurupuka na kudhani, pengine, kuwa mnakwenda mlikokwenda mara ya mwisho ambako hakukuona kwa maana.
Hata hivyo, kama kuna mtu anadhani ameishakumbana na maswali ya aina hii, asijidhanie kuwa wa kwanza wala wa mwisho, kwani mwanamke anazo njia nyingi za kumjaribu mwanaume kuangalia kama kweli anampenda na amedhamiria kuwa naye daima.
Kanuni ya msingi ya kutumia unapojikuta katika hali hii ni kumpa changamoto mwanamke, hadi kufikia hatua yeye akawa katika wasiwasi wa kukupoteza. Kwa ujumla, usikubali kila mara kuwa mtu wa kujitetea na kulazimika kutoa majibu ya kujisafisha kwa mwanamke.
Hakikisha kuwa mwanamke ndiye anayekuwa katika hali ya kuchanganyikiwa kutokana na msimamo wako, badala ya wewe kuchanganyikiwa kutokana na majibu yake, kwani wanawake hawana majibu ya moja kwa moja.
Kama, mathalani, kwa kuzingatia mfano ulioelezwa hapo juu, mwanamke ameahirisha mtoko halafu akawa anakuuliza maswali ya kijinga, basi kuna kila dalili kuwa alipokwambia ameahirisha ulifadhaika au kukasirika.
Kwa hakika karibu kila mwanaume atakuwa na mabadiliko akikataliwa mtoko, hasa kama alikuwa na maandalizi makubwa ya kimwili, kisaikolojia na kifedha, tena zaidi kama amebadilisha mawazo katika dakika za mwisho (kama wafanyavyo mara kwa mara).
Lakini hali itakuwa mbaya zaidi kama mwanamke mwenyewe anautesa moyo wake na ilikuwa iwe mara yako ya kwanza kujivinjari naye viwanja.
Lakini katika hali kama hiyo pamoja na hali nyingine ambapo mwanamke anaonesha kutokukujali kwa kadiri unavyomchukulia, unapaswa kujitokeza kama mtu asiyetetereka, ukionesha kutoshtuka, ukiendelea kujiamini. Kamwe usimwoneshe mpenzi wako, au mpenzi wako mtarajiwa, kuwa kitendo chake cha kukupuuza kimekuuma.
Baada ya kukabiliana na hali hii kwa mara ya kwanza, siku nyingine mpenzi wako (au msichana unayemfukuzia) akikupiga chini dakika za mwisho ukiwa naye ana kwa ana, hakikisha kuwa humwoneshi kuwa umefadhaishwa na hatua yake kwa namna yoyote ile na ikiwezekana waweza kumwonesha kuwa kumbe kuvuja kwa pakacha kumekuwa nafuu kwa mchukuzi, kwa kumwambia kuwa wewe pia una shughuli nyingine muhimu ya kufanya jioni au siku hiyo na kwamba amekusaidia sana.
Lakini kama kwa sababu yoyote ile mwanamke ataendelea kukuuliza maswali ya kijinga baada ya kukuumiza, mathalani akakuuliza kama hujisikii vizuri, mjibu kwamba ni kinyume cha mawazo yake, kwani kwa hakika umejisikia kutua mzigo.
Unapoyasema hayo, usionekane kukasirika, bali onesha tabasamu na kicheko, japo ndani unaweza kuwa unajihisi kuumia.
Mwache mwanamke akijiuliza umemaanisha nini hasa kwa kusema kuwa umetua mzigo, au hata kwa kuonesha kuwa hukuumia. Kumbuka kuwa msichana huyu alifahamu tangu awali kuwa asingekuwa tayari kutoka na wewe siku hiyo kwa hiyo hatua yake haikuwa ya bahati mbaya, bali ina malengo.
Kwa msichana aliyekweleza kuwa anahisi kutoka ni kupoteza muda, ni dhahiri kuwa mapenzi yake kwako yatakuwa madogo. Mwanamke anayekupenda kwa dhati hawezi kudhani kutoka na wewe ni kupoteza muda.
Lakini hata hivyo, anapokutamkia kauli hiyo nia yake ni kukuweka katika shinikizo. Kwa hiyo, kama kawaida, mgeuzie kibao kwa kuelekeza changamoto kwake. Kama, mathalani atasema, "Sitaki unipotezee muda. Kweli huna mwanamke mwingine?" Mwambie: "Mpenzi, huwezi kupoteza muda ukiwa na mimi." Maswali yake mengine yajibu kwa majibu muafaka pia.
La muhimu ambalo mwanaume anapaswa kulifahamu ni kwamba, njia nzuri zaidi ya kuishi na mwanamke ni kumfanya kila mara aendelee kuwa na shaka kuhusiana na mawazo yako, asije akautumia udhaifu wako kukunyanyasa.
Wanaume wengi hujikuta wakitumia nguvu nyingi kuwabembeleza wanawake kwa ajili ya mambo mbalimbali na kwa kufanya hivyo hujikuta wakichezewa na wanawake wasiokuwa na mapenzi ya dhati kwao.
Lakini siri kubwa ya kufanikiwa katika mapenzi ni pamoja na kumwacha mwanamke katika hali ambayo kila mara anataka kufahamu zaidi kuhusiana na msimamo wako na njia mojawapo ya kufanya hivi ni kutoa majibu muafaka kwa maswali muafaka.
Kama mwanamke unayemfukuzia hajaonesha kuvutiwa sana nawe, itakuwa rahisi kwake kukukimbia atakapobaini kuwa kumbe huna msimamo na unaweza kuyumbishwa na kufadhaishwa kwa jambo dogo, kama kuahirishiwa tarehe ya mtoko.
Lakini kama amevutiwa nawe, msimamo wako na kujiamini kwako vitampa changamoto kiasi cha kujihisi kuwa atakuwa amepata hasara kwa kumkosa mwanamume wa aina yako.

KWA mtu ambaye ndiyo kwanza anajiingiza katika ulimwengu wa mapenzi, ni dhahiri kuwa atakutana na mambo mengi ya kumkwaza, ambayo hatimaye yanaweza kumvunja moyo kuhusiana na suala zima la mapenzi. Wanaume, hususan kwa kuwa ndio wenye jukumu la kuanzisha mahusiano, hujikuta katika wakati mgumu wanapokwenda kukabiliana na wanawake, kutokana na tabia za wanawake, hasa wasichana za kutaka kujilinda.

Wanaume wengi wamekata tamaa na kubaki wakinung'unika, kutokana na kusalimu amri kwa makwazo mbalimbali yatokanayo na tabia ya asili ya mwanamke, ya kumjaribu mwanaume.

Mojawapo ya makwazo ambayo huweza kumkuta mwanaume katika uwanja wa mapenzi ni maswali ya 'kijinga' ambayo mwanamke anaweza kumuuliza, kwa ajili ya kuangalia msimamo wake. 
Soma zaidi