| SIRI KUMI AMBAZO ZITAISUMBUA AKILI YA MWANAMKE |
|
|
|
| Written by Christian Hall |
| Thursday, 29 April 2010 05:54 |
|
MWANAMKE uliye naye ni mrembo, maridadi na mcheshi. Kwa hakika ni mkamilifu kwako na anatimiza ndoto za ujana wako kuhusiana na mwanamke umtakaye. Lakini, japo ukweli huuma, kuna uwezekano kuwa mwanamke huyu hakuwa mkamilifu huko nyuma, bali yamkini amepitia mambo mbalimbali yakiwamo yale ambayo usingependa kuyasikia.
Yawezekana kabla ya kukutana na wewe, mwanamke huyu alikuwa mtu mwingine tofauti kabisa, na pengine amefanya mambo yenye madhara kwake au kwa wengine na mambo haya yataendelea kumsuta mpenzi huyu maisha yake yote. Isipokuwa, hatataka ufahamu kuwa kuna jambo alilofanya huko nyuma ambalo sasa linamsuta. Pengine hofu kuu ya mwanamke huyu ni kwamba siku moja unaweza kuufahamu ukweli kuhusiana na maisha yake. Anafahamu kuwa ukifahamu basi uhusiano wenu utakuwa kwenye matatizo. Na yeye ndio ameshafika na asingependa kuachana na wewe. Yawezekana siku za nyuma, mwanamke huyu alikuwa mkarimu kwa wote katika suala la mapenzi. Lakini pia inawezekana alijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. Ilimradi tu, yapo mambo ambayo mwanamume asingependa kufahamu kuwa mpenzi wake aliyafanya. Yafuatayo ni mambo ambayo yamkini mwanamke aliyafanya siku za nyuma na asingependa ufahamu. 1. ALITEMBEA NA BOSI, MWALIMU Kuna uwezekano kuwa mpenzi wako wakati fulani alilazimika kutoa penzi ili mambo yake yaweze kwenda vizuri, na pengine ndiyo maana ana mafanikio fulani unayoyaona. Pengine alifanya mapenzi na bosi wake ili aweze kupata wadhifa, kupandishwa cheo au kuua “soo” fulani iliyojitokeza kazini. Lakini pia inawezekana alilazimika kufanya mapenzi na mwalimu wake wa chuo ili kuweka sawa somo fulani alilofanya vibaya. Vyovyote vile ilikuwa, ni wazi kuwa mpenzi wako atakuwa alilazimika kufanya mapenzi kwa ajili ya manufaa fulani. Kwa nini ana wasiwasi kuhusiana na hili, kwamba unaweza kulibaini? Mwanamke huyu anafahamu kuwa ukifahamu siri hii si tu utamwona hana maana na hana msimamo, lakini pia utamchukulia kuwa ni mwanamke anayeweza kufanya lolote ili apate kile akitakacho. Pia anafahamu kuwa ukifahamu hili atapa ugumu kuruhusiwa kwenda kwenye tafrija za kiofisi na nyinginezo. 2. ALIWAHI KUVALISHWA PETE YA UCHUMBA Yamkini unafahamu kuwa ulipokutana kimwili mara ya kwanza na mpenzi wako hukumkuta akiwa bikira. Hili halina tatizo kwa wanaume wengi wa sasa, maana wao ndio wahusika wakuu wa kuondoa bikira za wasichana. Lakini pamoja na hayo, pengine usingependa kusikia kuwa mwanamke wako aliwahi kuvalishwa pete ya uchumba na mwanamume mwingine huko nyuma. Kama mwanamke wako analo jambo hili maishani mwake, ni wazi kuwa wakati fulani alishakuwa tayari kuwa mke wa mtu mwingine ambaye si wewe. Mwanamke wako hatataka ujue hili, kwani ukijua, ile dhana uliyo nayo kwamba aliumbwa kwa ajili yako itapungua uzito au kuondoka kabisa, maana alikuwa aolewe na mwingine. Lakini pia hii inaweza kuanza kukusababisha uanze kumfikiria vibaya huyo mwanamume mwingine hata kama humjui. Mathalani, utataka kufahamu alikuwaje na kama alikuwa na fedha na hali nzuri zaidi yako au la. Pia utataka kufahamu ni kwa nini mambo yao yalikwama. 3. ZAMANI ALIKUWA MNENE SANA Yawezekana mwanamke wako yuko katika umbo unalolitaka wewe, umbo la ki-miss, au umbo la kawaida lisilo la kunenepa sana. Lakini, yawezekana zamani alikuwa mnene, amepungua karibuni tu. Mwanamke hatapenda sana uujue ukweli huu na ndiyo maana hata picha zake za unene amezitupa au kuzificha. Hii ni kwa sababu pengine hapendi kukumbuka jinsi alivyokuwa anatisha, au pengine asingependa kukutia wasiwasi kwamba siku moja anaweza kuwa mnene kiasi hicho. 4. ALIWAHI KUANGUKA KIFAFA, KUZIMIA Kuna uwezekano kuwa mpenzi wako zamani aliwahi kukumbwa na tatizo, pengine la kuanguka kifafa, au pengine aliwahi kuanguka na kuzimia. Kwa kuzingatia hulka yake, anaweza asipende ufahamu ukweli huu kuhusiana na maisha yake ya zamani. Yawezekana alikuwa mdogo tu, au pengine ni wakati alipokuwa anasoma, lakini hatapenda ulifahamu jambo hili, kwani anajua siku ukilifahamu unaweza kuyaunganisha mambo mengi na tukio hilo hata kama lilikuwa tatizo la siku moja ambalo haliwezi kutokea tena au kama ulikuwa ugonjwa ulishapona. 5. AMEWAHI KUTUMIA DAWA ZA KULEVYA Kuna uwezekano katika zama hizi kwamba mpenzi wako zamani alikuwa akijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. Ndiyo, wapo wasichana wengi ambao huonekana kwenye vyombo vya habari wakishuhudia maisha yao ya matumizi ya dawa za kulevya. Kama aliwahi kujihusisha na hilo , hatataka ufahamu. Mpenzi wako anaweza kuwa hakujihusisha sana, pengine kutokana na ujana tu alijaribujaribu, lakini hakuendelea. Hata hivyo, hatataka ufahamu, kwani anajua kuwa ukifahamu, basi tukio lolote la “uchizi” utalihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. 6. AMEWAHI KUFANYA UHALIFU Wanawake nao wanaweza kuwa wahalifu na kuna uwezekano kuwa mpenzi wako zamani alikuwa mhalifu, hata kama si uhalifu wa kutumia silaha. Kama alikuwa mhalifu, hata kama ni uhalifu wa kuwatukana watu, hatataka uifahamu rekodi yake hii, kwamba aliwahi kusimamishwa kizimbani na kuhukumiwa kwa kutukana. Katika jamii yetu, kufikishwa mahakamani kwa uhalifu wowote hakuleti picha nzuri, maana sasa utaanza kuhoji uadilifu wake. Tatizo hili lina uwezekano mkubwa wa kumfanya mpenzi wako kujitahidi kukufurahisha kwa kila jambo maana asingependa kutiliwa shaka. 7. ALIFANYA MAPENZI KATIKA NJIA ISIYO KAWAIDA Mojawapo ya siri ambazo mwanamke wako atazificha na kuhakikisha kuwa huzijui ni iwapo aliwahi kufanya mapenzi katika njia ambazo si za kawaida sana. Pengine aliwahi kufanya mapenzi kwenye gari na dereva wa shirika/kampuni, au aliwahi kufanya mapenzi ya watu watatu (wanawake wawili na mwanamume mmoja, au wanaume wawili, yeye mwenyewe). Au, inawezekana aliwahi kufanya mapenzi ya kisagaji, au kuingiliwa kinyume cha maumbile. Vyovyote vile itakavyokuwa ilitokea, mwanamke huyu atakuwa na wasiwasi kuwa siku ukigundua heshima yake itashuka. Ni mzigo ambao ataendelea kuubeba kichwani mwake huku akisali usije kufahamu. 8. ALIPIGWA PICHA AKIFANYA NGONO Katika jamii yetu sasa, kama zilivyo jamii za kimagharibi, maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano yamesababisha kuzagaa kwa picha za ngono kwenye intaneti au katika simu za mikononi. Yawezekana mpenzi wako zamani aliwahi kujisahau alipokutana na mwanamume asiyejali utu wa mwanamke, akamlewesha na kumpiga picha, kisha akaziweka katika blog au kuzihifadhi kwenye kadi yake ya simu. Lakini huyo huyo ndiye uliyekutana naye, ukampenda na sasa ni mama wa watoto wako. Tatizo atakalokuwa nalo mpenzi wako huyu ni kwamba si tu kwamba alifanya uhuni, lakini pia kuna kumbukumbu ya uhuni wake huo. Na kama picha hizo ziliwekwa katika mtindo wa video ndio kabisa. Mwanamke huyu anafahamu kuwa siku ukiziona ndio mwisho wa uhusiano wenu. 9. ALIFANYA NGONO NA MTU WAKO WA KARIBU Umewahi kujiuliza ni kwa nini rafiki yako huwa anamwonesha mpenzi wako tabasamu kubwa? Au je, umewahi kumwona mpenzi wako akikosa amani anapokuwapo kaka yako? Amini usiamini, kuna uwezekano kuwa huko nyuma, kabla hujakutana naye, mpenzi wako aliwahi kujirusha na mtu wako wa karibu, pengine kaka yako au rafiki yako. Mbaya zaidi, anaweza kuwa aliwahi kuwa na baba yako. Kama kuna mambo ambayo yatamsumbua sana akili mpenzi wako ni hili, kwani anafahamu kuwa watu hao aliowahi kuwa nao wanaweza kumwanika. Lakini pia ana wasiwasi kuwa unaweza kufahamu na anajua ukifahamu thamani yake itapungua sana, maana hutamchukulia tena kuwa wako, bali cha wote. Na huu pia unaweza kuwa mwisho wa uhusiano wenu. 10. ALIWAHI KUWA JAMVI LA WAGENI Hii sasa ndiyo siri kubwa zaidi ambayo iwapo atalazimika kusema siri zake zote basi hii ataisema ya mwisho: Kwamba ametembea karibu na kila mtu hapo jirani kiasi cha kuchukuliwa kama jamvi la wageni na pengine ametoa mimba kadhaa kabla hajakutana na wewe. Huu ni ukweli utakaomtia mwanamke aibu maisha yake yote. Ulipokutana naye ulikuta ameshabadilika, amekuwa malaika, lakini kumbe zamani alikuwa shetani. Hatapenda uufahamu ukweli huu maana ataharibu jina lake na sifa yake mbele yako. Mwanamume yeyote akifahamu mwanamke wake alikuwa hivi zamani atamtoa maana. USIPEKUE SIRI ZAKE Hujaambiwa uanze kufukua siri za mpenzi wako ili uweze kuzifahamu. Kumbuka wewe mwenyewe unazo siri zako ambazo usingependa mpenzi wako azifahamu. Isipokuwa, fahamu tu kuwa yapo mambo ambayo mpenzi wako aliyafanya zamani na asingependa ufahamu. Badala ya kumfuatilia, jikite zaidi katika hali yake ya sasa uliyomkuta nayo, akiwa mzuri, mpole, mwenye heshima, mwenye upendo kwako na aliyejitoa kwako. Chukulia yaliyopita kuwa si ndwele, ganga yaliyopo na yajayo. |






![]() | Today | 124 |
![]() | Yesterday | 211 |
![]() | This week | 124 |
![]() | Last week | 1478 |
![]() | This month | 875 |
![]() | Last month | 8325 |
![]() | All days | 15306 |
Your IP: : 38.107.191.86
,
Today: September 05, 2010
Powered by Business Times Ltd Valid XHTML and CSS.









