Sunday 05th of September 2010
|
Written by Erasto Stanslaus
|
|
Saturday, 24 July 2010 15:50 |
|
Na Chausiku Omary MANENO aliyoyatoa Kocha Msaidizi wa Simba, Syllersaid Mziray ni ishara tosha kuwa amewamaliza kabisa watani wao jadi, Yanga. Mziray ameanza kuifundisha Simba, mwanzoni mwa wiki hii na tayari ametoa kauli kali kwa watani wao wa jadi watakaokutana nao Agosti 14 katika mchezo wa Ngao ya Jamii. Kocha huyo mkongwe katika medani ya soka nchini amesema kwa kikosi alichokikuta Simba, Yanga wataumia watake wasitake. “Kwa kikosi hiki, Yanga waandike wameumia kwani sidhani kama watapata ushindi katika michezo yote mitatu, tutakayokutana nayo msimu ujao,” alisema Mziray. Mziray ambaye ni mtaalamu wa viungo aliongeza: “Nina wiki moja na timu lakini kabla kukutana na Yanga, kikosi changu kitakuwa kinatisha sana, nawaonea huruma watani wetu wa jadi kukutana nao Agosti 14”.
Mziray alisema hakushiriki katika usajili wa timu hiyo lakini kamati ya usajili imefanya kazi nzuri kwani kikosi hicho kimekamilika kila idara. Katika hatua nyingine, wanachama wa klabu hiyo wameutaka uongozi wao kuachana na Kocha wao, Patrick Phiri, kwani anachelewesha programu ya timu hiyo. Mmoja wa wanachama hao aliyejitambulisha kwa jina la Ali Bia alisema kitendo kinachofanywa na Phiri ni sawa na hujuma kwa timu hiyo. “Kama wamempata Mziray na ameanza kazi ni bora waendelee naye kwani kubadilisha makocha ina matatizo yake na itawavuruga wachezaji wao hatimaye kuboronga katika ligi msimu ujao,” alisema Ali Bia. Uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu' uliwahi kutoa kauli kuwa kama Phiri ataendelea kupiga danadana wataachana naye kabisa. |
Powered by Business Times Ltd
Valid XHTML and CSS.