|
Hispania yaweka Historia. |
|
Monday, 02 July 2012 04:41 |
|
|
Timu ya taifa ya Hispania jana usiku iliweka historia kwa kuwa timu ya kwanza kutwaa kombe la Euro mara mbili mfululizo, kwa kuifunga Italia magoli 4-0 katika fainali ya Euro 2012 mjini Kiev, Ukraine.
Licha ya mchezo mzuri wa Italia, vijana wa meneja wa Uhispania, Vicente del Bosque walithibitisha kwamba kimataifa wanaweza kujigamba wao ndio wenye mchezo bora zaidi duniani, kwa kuzingatia namna walivyoichezea timu ya Italia, na kuwalazimisha kusalimu amri.
David Silva aliifungia Uhispania bao la kwanza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Fabregas, na kabla nusu ya kwanza ya mchezo kumalizika, mchezaji mpya wa Barcelona, Jordi Alba aliandikisha bao la pili, baada ya kukimbia kwa kasi na kumalizia kwa ustadi pasi ya Xavi.
Fernando Torres aliyeingia akitokea benchi aliifungia Hispania goli la tatu kabla ya kumtengenezea Juan Mata goli la nne.
Ilikuwa ni fainali ambayo ilimvunja moyo kabisa kocha wa Italia, Cesare Prandelli, lakini bila shaka haikuwa fedheha kushindwa na timu yenye maarifa ya hali ya juu kama Hispania.
Italia itaweza kujivunia namna ilivyofika katika fainali, licha ya kushindwa kwa magoli mengi na timu ambayo ilikuwa ni wazi imo katika kiwango cha pekee.
|