|
Hispania yatinga fainali Euro 2012 |
|
Thursday, 28 June 2012 06:23 |
|
|
Mabingwa watetezi wa kombe la Euro Uhispania wamefuzu kuingia fainali ya Euro 2012, baada ya kuishinda Ureno magoli kwa penati 4-2.
Timu hizo zilifikia hatua ya kupigiana mikwaju ya penati baada ya muda wa kawaida wa dakika 90 na kisha 30 za ziada kumalizika kwa timu hizo mbili kushindwa kufungana.
Bao la mwisho la mikwaju ya penalti kwa Uhispania lilitiwa wavuni na Cesc Fabregas, na kuwapa wenzake matumaini ya kutetea ubingwa wao watakapocheza aidha na Ujerumani au Italia katika fainali ya Jumapili.
Xabi Alonso alikuwa wa kwanza kukosa penati baada ya golikipa wa Ureno Rui Patricio kuipangua penati. Kiungo wa Ureno Joao Moutinho naye alikosa penati ya kwanza ya Ureno baada ya kudakwa na Casillas.
Wafungaji wa penati za Uhispania walikuwa Pique, Ramos, Iniesta na Fabregas. Kwa upande wa Ureno Pepe na Luis Nani walifunga penati zao wakati beki Bruno Alves alipiga penati iliyogonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani.
|